IQNA

Ayatullah Hashemi Shahroudi wa Iran ameaga dunia

11:15 - December 25, 2018
Habari ID: 3471785
Ayatullah Sayyid Mahmoud Hashemi Shahroudi, mwanazuoni maarufu wa Kiislamu nchini Iran ameaga dunia baada ya umri uliojaa baraka.

Ayatullah Shahroudi, amefariki dunia jana Jumatatu, Disemba 24, 2018 akiwa na umri wa miaka 70 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Wakati wa kifo chake, Ayatullah Shahroudi alikuwa mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia aliwahi kuwa pia mjumbe wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha aliwahi kuhudumu kama mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Iran kwa muda wa miaka 10. Ayatullah Shahroudi pia alikuwa mwanachama wa  Baraza la Wanazuoni linalomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran na kusimamia kazi zake.

Ayatullah Sayyid Mahmoud Hashemi Shahroudi alizaliwa tarehe 15 Agosti 1948 katika mji wa Najaf nchini Iraq na alikuwa miongoni mwa wanafunzi wakubwa wa Shahid Ayatullah Sayyid Muhammad Baqir.

Baba yake yaani Ayatullah Sayyid Ali Husaini Shahroudi alikuwa mmoja wa wanavyuoni wakubwa wa Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf huko Iraq. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Hashemi Shahoroudi alishiriki pia katika darsa za Imam Khomeini MA na Ayatullah Khoui.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Shahroudi na kusema amesikitishwa na kifo chake na kumtaja  kuwa mwanazuoni aliyeandika vitabu vingi vyenye manufaa  kwa lengo la kuinua utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na Iran.

Aidha amemtaja kuwa mwanazuoni aliyejitahidi kukurubisha vyuo vikuu vya kidini vya vyuo vikuu vya kawaida na pia alijitahidi kustawisha sayansi za kijamii ambapo katika fremu hiyo aliasisi Chuo Kikuu cha Edalat mjini Tehran.

3775355

captcha