IQNA

Wabaguzi Waliomtusi Difenda Msenegal wa Napoli wapata darsa ya Qur'ani

19:04 - December 29, 2018
Habari ID: 3471790
TEHRAN (IQNA)- Mchezaji soka Msenegali ameashiria aya ya Qur'ani Tukufu kumtetea Kalidou Koulibaly Msenegali mwenzake ambaye ni difenda wa Timu ya Soka ya Napoli katika Ligia ya Italia ambaye amekumbana na matusi ya kibaguzi kutoka kwa mashabiki.

Akimtetea mwenzake aliyebaguliwa, Demba Ba ametumia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kuandika aya ya 13 ya Surah al-Hujurat isemayo: "Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari."
Demba Ba ambaye ni mchezaji wa kulipwa Msenegal ambaye ni mshambuliaji wa Klabu ya Shanghai Shenhua ya China mbali na kuwa mchezaji wa timu ya taifa ya soka ya Senegal.
Jumatano iliyopita, Kulibali alilengwa kwa matusi ya wabaguzi wa rangi baada ya timu yake kupoteza 1-0 katika mechi na Inter Milan katika Ligi Kuu ya Italia, Serie A. Shirikisho la Soka Barani Ulaya, UEFA, limelaani vikali ubaguzi huo na kuutja kuwa 'usiokubalika'.
Mashabiki wa Inter Milan walianza kupaza sauti zinazoshabihiana na sila za wanyama huku wakitumia matusi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Koulibali wakati wa mechi hiyo.
Wakuu wa Serie A Ijumaa walichukua uamuzi wa haraka wa kuiadhibu timu ya Inter Milan kutokana na vitendo vya kibaguzi vya mashabiki wake ambapo mechi mbili zijazo za nyumbani za timu hiyo zitachezwa pasina kuwepo mashabiki. Jumuiya ya kimataifa ya wachezaji wa kulipwa, FIFPro na UEFA zimetoa taarifa ya pamoja na kuwashukuru wasimamizi wa Serie A kwa hatua za haraka walizochukua huku wakisisitiza kuwa matusi hayana sehemu yoyote katika soka.
Kocha wa Timu ya Chelsea ambaye aliwahi kuwa kocha wa Napoli, Maurizio Sarri, ameitaka Itali ichukue hatua za kukabiliana na ubaguzi katika soka nchini humo.

/3776407

captcha