IQNA

Mufti Mkuu wa Russia

Russia inahitaji misikiti zaidi kutokana na ongezeko la Waislamu

18:10 - March 05, 2019
Habari ID: 3471862
TEHRAN (IQNA)- Waislamu wanatarajiwa kuongezeka na kufika asilimia 30 ya watu wote wa Russia ifikapo mwaka 2034 na hivyo kuna haja ya kujenga misikiti zaidi nchini humo.

Hayo yamedokezwa na  Mufti Mkuu wa Russia Sheikh Ravil Gainutdin alipokuwa akihutubu katika kongamano moja mjini Moscow Jumatatu ambapo amebainisha kuwa Waislamu wamekuwa wakiongezeka kila siku nchini humo.

"Kwa mujibu wa makadirio ya wataalamu, asilimia 30 ya watu wote Russia watakuwa ni Waislamu katika kipindi cha miaka 15 ijayo," amesema Sheikh Gainutdin.

Amekumbusha kuwa, mwaka uliopita, Waislamu wapatao 320,000 mjini Moscow walishiriki katika  Sala ya Idul Adha na kuongeza kuwa, idadi hiyo ilikuwa ni rekodi mpya.

Mufti wa Russia amesema idadi kubwa ya waumini wanaoshiriki katika Sala za Idi ikilinganishwa na miaka iliyotangulia, ni ishara ya ongezeko la Waislamu nchini humo.

Aidha amesema kuna haja ya kujenga misikiti mipya katika miji mikubwa ya Russia huku akiongeza kuwa idadi ya Waislamu nchini Russia ni milioni 25. Idadi ya watu wote Russia ni takribani milioni 144 na aghalabu ni Wakristo wa madhehebu ya Orthodox.

Mufti wa Russia anasema sababu kuu ya ongezeko la Waislamu ni idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa katika familia za Kiislamu na pia wahajiri kutoka Asia ya Kati.

Russia inahitaji misikiti zaidi kutokana na ongezeko la Waislamu

Sala ya Idi katika Msikiti wa Moscow

Russia inahitaji misikiti zaidi kutokana na ongezeko la Waislamu

Mufti Mkuu wa Russia Sheikh Ravil Gainutdin  akihutubu katika Msikiti wa Moscow

/3795355

captcha