IQNA

Rais wa Iran: Waislamu Warohingya warejeshwe haraka nchini Myanmar

19:09 - March 09, 2019
Habari ID: 3471869
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuhusu kuwepo uthabiti na amani nchini Myanmar. Aidha amesisitiza kuwa wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya warejeshwe haraka na kwa usalama katika makazi yao nchini Myanmar.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo Jumamosi mjini Tehran wakati alipopokea vitambulisho vya Mukyu Ung, balozi mpya wa Myanmar nchini Iran. Rais Rouhani amesema uthabiti na usalama katika nchi yoyote hupatikana kwa kushirikiana watu wa kaumu na jamii  zote, ameelezea matumaini kuwa: "Jitihada za serikali ya Myanmar zitazaa matunda na uthabiti na usalama utarejea nchini humo ili wakimbizi waweze kurejea katika nchi yao."

Rais Rouhani pia amesema kuna uwezekano wa kuimarishwa uhusiano wa Iran na Myanmar na kuongeza kuwa: "Nchi mbili zinaweza kushirikiana katika nyanja kama vile huduma za uhandisi, uwekezaji, biashara na utalii."

Kwa upande wake, Mukyu Ung, balozi mpya wa Myanmar nchni Iran ameishukuru Iran kwa kuwa na uhusiano mzuri na nchi yake.

Kuhusiana na hali ya Waislamu wa jamii ya Rohingya, Mukyu Ung amesema: "Serikali ya Myanmar inajitahidi kuchukua hatua za kuwarejesha wakimbizi katika maeneo yao na kuhusiana na hilo kuna mapatano yaliyofikiwa na Bangladesh pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa."

Tokea Agosti 25 2017 wakati Jeshi la Myanmar lilipoanzisha hujuma dhidi ya Waislamu katika jimbo la Rakhine, Waislamu zaidi ya elfu saba wameuawa kwa umati na makumi ya maelfu ya  wengine elfu nane wamejeruhiwa.

Kufuatia hujuma hizo Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za jirani kutokana na mashambulio ya Mabuddha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo. Kuna karibu Waislamu milioni moja wa jamii ya Rohingya waliokimbilia hifadhi nchini Bangladesh.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, imesema inatafakari kuhusu kuanzisha uchunguzi kuhusu ukatili wanaotendewa Waislamu wa jamii ya Rohingya.

3468091

captcha