IQNA

Wapinzani Sudan watangaza mpango wa kuunda baraza la mpito

14:22 - June 11, 2019
Habari ID: 3471995
TEHRAN – (IQNA)- Muungano wa makundi ya upinzani yanayoongoza vugu vugu dhidi ya utawala wa kijeshi Sudan umetangaza mpango wa kuteua watu wanane katika baraza la mpito katika nchi hiyo ambayo inakumbwa na msukusuko mkubwa wa kisiasa.

Katika taarifa, Muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko umetangaza kumteua Abdullah Hamdouk, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa barani Afrika kuwa Waziri Mkuu wa serikali ijayo ya mpito. Aidha muungano huo umewateua wanawake watatu kuwa wanachama wa baraza hilo.

Tangazo hilo limetolewa Jumatatu katika siku ya pili ya kampeni ya uasi wa kiraia wa nchi nzima iliyoanza siku ya Jumapili nchini Sudan. Taarifa zinasema watu wanne wameuawa na maafisa usalama katika siku ya kwanza ya kampeni hiyo.

Kadhalika kampeni hiyo ya uasi wa kiraia imepelekea mji wa Khartoum na miji mingine mikubwa ya nchi kusalia mahame, huku maduka na vituo vingi vya biashara vikifungwa.

Kwingineko, Shamsuddin al Kabbashi, Msemaji wa Baraza la Kijeshi la Serikali ya Mpito ya Sudan ametangaza kuwa baraza hilo liko tayari kufanya mazungumzo bila ya masharti na Muungano wa Uhuru na Mabadiliko wa nchi hiyo, kwa lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.

Hata hivyo Muungano wa Uhuru na Mabadiliko wa Sudan umesema kuwa ili kuendelea kufanya mazungumzo na Baraza la Kijeshi kuna udharura wa kuundwa kamati ya kimataifa ya kuchunguza mauaji ya makumi ya watu wakati askari usalama walipowavamia wapinzani waliokuwa katika mgomo wa kuketi chini mjini Khartoum.

Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan ulishadidi Juni 3 baada ya wanajeshi kuwashambulia waandamanaji waliokuwa wamekusanyija nje ya makao makuu ya jeshi ambapo raia zaidi ya 100 waliuawa katika vurumai hiyo.

Wakati huo huo tovuti ya Middle East Eye imefichua kwamba, Kiongozi wa Baraza la Kijeshi la Mpito huko Sudan Jenerali Abdel Fattah al Burhan aliidhinishwa na Saudi Arabia na waitifaki wake kufanya mashambulizi hayo dhidi ya raia waliokuwa wamekusanyika na kufanya mgomo mbele ya makao makuu ya jeshi la nchi hiyo.

Zaidi ya raia mia moja wameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa katika mashambulizi ya hivi karibuni kabisa ya jeshi la Sudan dhidi ya raia wanaoandamana kupinga utawala wa kijeshi.

Mgogoro wa Sudan uliibuka Disemba mwaka jana baada ya wananchi kumiminika mabarabarani wakilalamikia hali mbaya ya kiuchumi ambapo kufuatia maandamano hayo, tarehe 11 Aprili mwaka huu jeshi la Sudan lilitangaza kumuondoa madarakani Rais Omar al-Bashir na kutwaa madaraka ya nchi hiyo. Baada ya hapo jeshi hilo liliunda Baraza la Kijeshi la Mpito ingawa wananchi wanalipinga na kulitaka liruhusu kuundwa serikali ya kiraia.

Matukio ya nchini Sudan katika muongo mmoja uliopita yanaonyesha kuwa ajinabi wamekuwa wakiingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na hapa tunaweza kutaja nafasi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuivunja nchi hiyo katika vipande viwili vya Sudan na Sudan Kusini. Katika mgogoro wa hivi sasa wa Sudan pia, madola ajinabi yanaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ambapo Saudi Arabia na Imarati zimetajwa kuwa na nafasi kubwa katika kuliunga mkono jeshi ambalo linawakandamiza wananchi kwa lengo la kunyakua madaraka kikamilifu. Kuna ushahidi unaoashiria namna madola hayo mawili ya Kiarabu yanavyoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

/3468715

captcha