IQNA

Iran na Hamas zasisitiza:

'Muamala wa Karne' umetayarishwa na Marekani kwa maslahi ya Utawala wa Kizayuni

19:17 - June 16, 2019
Habari ID: 3472004
TEHRAN (IQNA) - Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) zimesema utawala wa rais Donald Trump wa Marekani unalenga kuangamiza taifa la Palestina kupitia 'Muamala wa Karne' ulio kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Asia Magharibi.

Hayo yamesemwa Jumapili mjini Beirut katika mkutano baina ya Waziri wa Usalama wa Taifa wa Iran Mahmoud Alavi na maafisa wa ngazi za juu wa Hamas mjini Beirut. Kwa mujibu wa taarifa walioshiriki katika mkutano huo ni Naibu Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Hamas Saleh Al-Arouri, mwanachama wa Idara ya Kisiasa ya hamas Hessam Badran, mkuu wa masuala ya kigeni katika Hamas Osama Hamdan na mwakilishi wa Hamas nchini Lebanon Ahmed Abdulhadi.

Kwa mujibu wa tovuti ya Hamas, katika mkutano huo, pande mbili zimesisitiza kuwa, sera ambazo Marekani inatekeleza zinabainisha wazi kuwa maamuzi ya kuunga mkono Israel ambayo yamechukuliwa na rais wa Marekani yanatazamiwa kuendelea kwa kuunga mkono hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kujenga vitongoji vya alowezi wa kizayuni katika Ukingo wa Magharibi na minuko ya Golan. Wamesema baadhi ya hatua ambazo Marekani imechukua katika kuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji huo.

Aidha pande mbili  zimejadili kuhusu kuimarisha uhusiano wa Iran na Hamas na ulazima wa mashauriano ya mara kwa mara ili kukabiliana na changamoto na hatari zitokanazo na sisitizo la Markenai la kutekeleza  'Muamala wa Karne' ambao umekataliwa na Wapalestina wote pamoja na mataifa ya kieneo.

Aidha pande mbili zimejadili njia za kukabiliana na njama za Marekani na Wazayuni katika eneo hasa kuhusu kadhia ya Palestina.

Mwezi Mei Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa "Muamala wa Karne" uliopendekezwa na Marekani kuhusu Palestina ni muamala muovu sana na kwamba kikao kilichopangwa kufanyika mwezi ujao huko Bahrain kujadili mpango huo nacho kitatumbukia kwenye moto wa jahannam kama ilivyo kwa muamala huo wa karne.

Rais wa Marekani, Donald Trump alipendekeza kwa mara ya kwanza mpango wa "Muamala wa Karne" mwaka 2017 na kuzishinikiza tawala za kifalme za Saudi Arabia, Bahrain na Imarati kugharamia fedha za mpango huo.

Kikao cha Bahrain ambacho kimetajwa kuwa ni hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mpango wa "Muamala wa Karne" kinatarajiwa kufanyika tarehe 25 na 26 mwezi huu wa Juni 2019 mjini Manama. Kikao hicho kimeitishwa kwa uungaji mkono wa baadhi ya tawala za kiimla za Kiarabu na moja ya malengo yake ni kuhakikisha nchi za Kiarabu zinakuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao mikono yake imejaa damu za watu wasio na hatia hasa Wapalestina.

3819834

captcha