IQNA

Marekani, Israel, Saudia zinaichochea Nigeria iendelee kumshikilia Sheikh Zakzaky

23:21 - July 21, 2019
Habari ID: 3472050
TEHRAN (IQNA) - Mashinikizo ya Marekani, Utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia ni chanzo kikuu cha serikali ya Nigeria kuendelea kumshikilia kinyume cha sheria kiongozi wa harakati ya Kiislamu nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky.
 
Duru zinadokeza kuwa, pamoja na kuwa Mahakama Kuu ya Nigeria imeagiza Sheikh Zakzaky aachiliwe huru kutokana na kuzorota afya yake, lakini serikali ya nchi hiyo imekataa kutii amri hiyo kutokana na mashinikizo ya tawala za Marekani, Israel na Saudia.
Wakati huo huo Waislamu na wanaharakati nchini Nigeria  Ijumaa waliendeleza maandamano ya kutaka kuachiwa huru Sheikh I Zakzaky, licha ya kukabiliwa kwa mkono wa chuma na maafisa usalama wa nchi hiyo.
Maandamano makubwa ya amani yalishuhudiwa jana katika jimbo la Katsina, kaskazini magharibi mwa nchi, ambapo waandamanaji wameiomba mahakama iruhusu Sheikh Zakzaky na mkewe waende wakatibiwe nje ya nchi.
Haya yanajiri katika hali ambayo, duru za kieneo zimetangaza kuwa, Mahakama Kuu ya Nigeria inachunguza uwezekano wa kuruhusiwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kwenda kutibiwa nchini India.
Wanaharakati wa mitandao ya kijamii nchini Nigeria jana Ijumaa walisambaza picha zinazoonesha Sheikh Zakzaky na mkewe wakiwa wamefungiwa katika chumba kimoja sehemu isiyojulikana.
Kwingineko, Chama cha Wahadhiri na Wanachuo wa Sayansi ya Tiba nchini Iran kimetahadharisha kuhusiana na hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Katika barua yao kwa ofisi yya Umoja wa Mataifa na ubalozi wa Nigeria hapa mjini Tehran, Chama cha Wahadhiri na Wanachuo wa Sayansi ya Tiba nchini Iran kimetaka kuachiliwa huru haraka Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeonyesha wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali ya kiafya ya kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu nchini Nigeria.
Kadhalika Chama cha Wahadhiri na Wanachuo wa Sayansi ya Tiba nchini Iran kimewataka maulama wa Kiislamu, wanaharakati wa masuala ya kiutamaduni na wa haki za binadamu kufuatilia kwa karibu hali ya matibabu ya Sheikh Ibrahim Zakzaky.
AIdha Sheikh Muhammad Jafar Montazeri Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwaandikia barua viongozi wa vyyombo vya mahakama vya Nigeria akilaani vikali hatua ya wanajeshi wa Nigeria dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, na kutoa wito wa kuachiliwa huru mwanazuoni huyo na kuletwa hapa Iran kwa ajili ya matibabu.
Mwaka 2015, jeshi la Nigeria lilivamia na kushambulia mkusanyiko wa Waislamu katika Husseiniyah ya Baqiyatullah huko Zaria kwenye jimbo la Kano na kuua shahidi kwa umati karibu Waislamu elfu moja. 
Sheikh Zakzaky mwenyewe na mkewe walipigwa risasi na tangu wakati huo wanashikiliwa katika korokoro za serikali ya Rais Muhammadu Buhari ambayo inaendelea kukaidi amri ya Mahakama Kuu ya kumwachilia huru mwanachuoni huyo.
3468997
captcha