IQNA

Jeshi Sudan kuchukua hatua baada ya wanafunzi kuuawa katika maandamano

10:32 - August 01, 2019
Habari ID: 3472066
TEHRAN (IQNA)- Jeshi la Sudan limetaka wahusika wachukuliwe hatua baada ya waandamanaji watano wakiwemo wanafunzi wanne kuuawa kwa kupigwa risasi katika maandamano ya jana nchini Sudan.

Mauaji hayo yametokea Jumatatu, siku moja kabla ya kuanza tena kwa mazungumzo kati ya utawala wa kijeshi na viongozi wa maandamano ikiwa ni katika juhudi za kufikia makubaliano ya mwisho kuhusu uongozi wa mpito.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, mji wa Al-Obeid, makao makuu ya Jimbo la Kordofan Kaskazini jana ulishuhudia maandamano makubwa. Duru za hospitali zinasema kuwa, waandamanaji watano wamepigwa risasi katika maandamano hayo ya amani.
"Kile ambacho kimefanyika Al-Obeid kinasikitisha na kuuawa raia ni jambo lisilokubalika na waliohusika wawajibishwe," amesema Abdel Fattah al Burhan, mkuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi Sudan.
Wanajeshi wa Sudan walichukua madaraka baada ya kupinduliwa Rais wa nchi hiyo Omar al Bashir Aprili 11 mwaka huu, hata hivyo wananchi wangali wanasisitiza kuhusu takwa lao la kuundwa serikali ya kiraia nchini humo.
Serikali ya Sudan imetangaza kufunga shule zote nchini humo kufuatia mauaji ya Al Obeid kwa kuhofia maandamano makubwa ya wananchi.

3469079

Kishikizo: sudan iqna
captcha