IQNA

Allamah Fadhlullah: Mapinduzi ya Iran ni kigezo cha utekelezaji wa Uislamu katika jamii

11:15 - December 06, 2008
Habari ID: 1716239
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kigezo bora cha utekelezaji wa mafundisho na misingi ya dini ya Kiislamu katika jamii ya ulimwengu wa Kiislamu na Imamu Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ambaye ndiye muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alitoa mitazamo yake ya kisiasa, kifikra na kiutamaduni kwa mujibu wa Uislamu na mahitaji ya zama hizi.
Hayo yamesemwa na Allamah Muhammad Hussein Fadhlullah mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu wa Lebanon mjini Makka. Sayyid Fadhlullah amesema: Maulama na viongozi wakuu wa vyuo vikuu vya kidini vya Najaf Iraq na Qum nchini Iran wametoa mchango muhimu katika harakati za Kiislamu za miaka ya hivi karibuni katika pembe mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Muhammad Hussein Fadhlullah ambaye alikuwa akizungumza na kiongozi wa ujumbe wa Hija wa Lebanon katika mji mtakatifu wa Makka amegusia pia matatizo ya sasa ya ulimwengu wa Kiislamu na akasema: Ibada ya Hija ina taathira kubwa katika mshikamano wa kisiasa na kiibada wa Waislamu na ni nguzo muhimu ya kuimarisha umoja wa Kiislamu na kujiepusha na chuki za kimadhehebu na kikaumu.
Ayatullah Fadhlullah ameongeza kuwa ni wajibu wa Waislamu wote kubainisha ujumbe wa Uislamu na kwamba wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu wanapaswa kuheshimu urithi wenye thamani kubwa wa dini hiyo kupitia njia ya mazungumzo na mawasiliano.
Amesema kuwa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah huko Lebanon ilifanikiwa kuzima njama za mabeberu wa kimataifa na utawala ghasibu wa Israel katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kutegemea Qur’ani na mafundisho ya Uislamu. Amesisitiza kuwa mbali na jihadi na mapambano ya kijeshi, katika kipindi cha sasa ulimwengu wa Kiislamu unahitajia pia mapambano ya kiutamaduni ili kuweza kukabiliana na njama za maadui, kubakia nyuma kimaendeleo, fikra potofu na mafundisho yasiyokuwa sahihi. 330079
captcha