IQNA

23:10 - March 29, 2016
1
News ID: 3470220
Tarehe 20 ya mwezi Jamaduthani mwaka wa Hijiria, mji wa Makkah huwa unanukia uturi wa ua la Jasmine. Hii ni kwa kuwa, tarehe hiyo inasadifiana na tarehe aliyozaliwa ndani yake Bibi Fatima Zahra AS, binti wa Mtume SAW ambaye alipewa lakabu ya 'mama wa baba yake' na 'kheri nyingi'.

Kwa mara nyingine tena nyumba ya Mtume inag’ara nuru ambayo inauangaza ulimwengu wote. Malaika wamesimama safu kwa safu wakisubiria idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ajili ya kushuka kwenye nyumba hiyo ya peponi kwa lengo la kutoa mkono wa baraka na salamu za Mwenyezi Mungu kwa mama wa binti huyo wa Mtume ambaye si mwingine bali ni Khadijatul-Kubra AS, mmoja wa wanawake wane wabora zaidi duniani. Mtume anasujudu sijda ya kushukuru huku macho, moyo na roho yake vikiwa vimejawa na urangi wa buluu kwa furaha. Mtume Muhammad SAW anamshukuru Mola wake Mtukufu kwa kumruzuku mtoto ambaye ni kiini cha fakhari na thamani ya ulimwengu na walimwengu kwa ujumla. Ni wakati huo ndipo unamshukia wahyi wa haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu ukisema: "Hakika sisi tumekupa kheri nyingi, basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje. Hakika mwenye kukubughudhi yeye ndiye aliyekatikiwa.” Surat Kauthar aya ya 1-3. Katika kipindi hiki wasikilizaji wapenzi hususan wapenzi wa kizazi cha Mtume, tunakusudia kuelezea kiini cha mapenzi ya Nabii huyo wa Allah SWT kwa mwanamke huyo mtoharifu yaani Bibi FatimaZahra AS hivyo endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Bibi Fatima Zahra AS ambaye ni binti ya Mtukufu Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni mwanamke wa kipekee ambaye alilelewa katika msingi wa malezi ya Kiislamu. Kupitia msingi huo alifikia kilele cha imani, utakatifu, maarifa, akhlaqi na fadhila mbalimbali za ubinaadamu, huku akifikia pia ukamilifu wa kimaanawi na daraja ya juu ya Allah. Uhusiano usio na mfano kati yake na Mtume wa Mwenyezi Mungu, ulishamili zaidi kupitia msingi wa imani na upendo. Hii ni kwa kuwa urafiki na mahaba ya mawalii wa Mwenyezi Mungu na watu walio karibu sana na Allah katika kuwapenda watu wengine hususan watoto wao, huwa yanatofautina sana na uhusiano wa watu wa kawaida. Mahaba na irada ya watu watakatifu haiegemei kwenye mahusiano ya nafsi na matamanio, bali husimama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana watukufu hao wakawa hawazingatii upendo ambao haujajengeka juu ya msingi wa Mwenyezi Mungu.

Mtukufu Mtume SAW, ni mja mwema wa Mungu ambaye hana mfano huku, maneno, mienendo na maisha yake yote vikienda sambamba na aya ya 3 na 4 ya Surat Najm. Ni kwa ajili hiyo ndio maana haifai kupuuza mafundisho ya hali ya juu ya Mtume kumuhusu mwanamke huyo ambaye ni kioo cha Uislamu, au pia kupuuza mienendo na miamala isiyo na mfano na yenye hekima na siri kubwa ambayo ilikuwa ikifanywa na Mtume SAW kwa Bibi Fatima AS. Hasa kwa kuzingatia kuwa, kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, Mtume alikuwa na mabinti wengine mbali na Fatimana ambao walikuwa wakubwa zaidi yake. Lakini pamoja na hayo, hakuna binti ambaye alibahatika kupata mahaba kama yale ambayo Mtume alikuwa akimpatia Bibi Fatima Zahra AS. Hakuna shaka kuwa hiyo ilitokana na kwamba, upendo huo ulitokana na wahyi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa mujibu wa historia, Mtukufu Mtume Muhammad SAW alikuwa akimuonyesha mwanaye huyo (Fatima) hisia zake zote za ubaba. Katika mimbar, na katika mihrab, katika sala, dua na maombi, mjini Makkah na Madina, ndani ya mji na nje yake, kwenye kila mlima na eneo tambarare, kwa watu wa karibu na wageni, alikuwa akimuheshimu binti yake huyo mtoharifu, na hata wakati alipokuwa akienda safari, mtu wa mwisho aliyekuwa akimuaga, alikuwa Bibi Fatima AS. Vitabu mbalimbali kama vile Musnad Imam Ahmad juzu ya 5, Sunan Abi Daud juzu ya pili, Sunan Kubra Bayhaqi juzu ya 1 na vinginevyo, vimeandika kuwa, wakati Mtume alipokuwa akirejea nyumbani, alikuwa akiubusu mkono wa FatimaAS. Katika kitabu cha Biharul-Anwaar juzu ya 43 imeandikwa kuwa, mtu ambaye anabusu mkono wa Fatwimah, naye Jibril hubusu udongo wa nyayo za miguu yake. Kwa ajili hiyo utaona ni kwa kiasi gani miamala hiyo ya Mtume (saw), haikusukumwa na mapenzi ya baba kwa mwanaye tu, bali vilisababishwa na uelewa na maarifa ya juu kwa Bibi Fatima Zahra AS. Wakati Mtume alipokuwa akiulizwa ni kwa nini alikuwa akifanya hivyo? Alikuwa akisema: ”Mimi ninahisi harufu ya pepo. Wakati ninapombusu Fatima basi hunikurubisha kwenye pepo.” Tazama kitabu cha Ilalush-Sharaiul-Anwaar juzu ya 1. Katika sehemu nyingine imeandikwa kuwa, Mtume alikuwa akiwajibu wale watu waliokuwa wakihoji ni kwa nini alikuwa akimuonyesha mapenzi Bibi Fatima Zahra zaidi ya mabinti wake wengine, kwa kusema kama ninavyonukuu: "Unayo haki ya kutofahamu siri yake! Kwa kuwa humumtambui Fatima! Fatima ananifanya niweze kufikia malengo, ananifanya niweze kuvumilia tabu na matatizo. Yeye ni sababu ya kusalia dini yangu. Ni sababu ya kulindwa uongozi na suna zangu.”

Sababu ya miamala ya Mtume na maneno hayo aliyokuwa akiyatoa kumuhusu mwanamke huyo, vilitokana na sifa aali na za ukamilifu zilizodhidhiri katika shakhsia tukufu ya Bibi Fatima Zahra AS. Aidha siri ya mapenzi ya Mtume kwa mwanamke huyo, ilikuwa na nafasi kubwa katika imani, uchaji-Mungu na ukamilifu wake. Kwa hakika mwanamke huyo alikuwa kiini cha ukamilifu huku akiwa amekusanya sifa zote za kumfanya aitwe mtu wa Mungu. Kuhusiana na suala hilo Mtukufu Mtume SAW anasema: "Wanawake wakamilifu kati ya wanawake wote, ni Maryam, Asia, Khadija na Fatwimah.” Tazama kitabu cha Durrul-Manthur juzu ya 2. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mtukufu Mtume akamuarifisha binti yake huyo, kuwa ni mwanamke aliyefikia ukamilifu wa adabu, matukufu yote ya daraja ya juu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, huku akiwa amefungasha pia matukufu ya akhlaqi, uchaji-Mungu na ubinaadamu. Ni mwanamke ambaye alikuzwa na matunda ya msitu wa utume, chemchemi inayopita ndani yake, fadhila na utukufu wake. Imam Khomein MA Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, aliielezea shakhsia ya juu ya mwanamke huyo kwa kusema: "Sifa zote zinazompamba mwanamke na kumuarifisha kama mwanadamu mkamilifu, zilikuwa nyuma zikilinganishwa na zile alizokuwanazo Bibi FatimaZahra AS. Hakuwa mwanamke wa kawaida. Alikuwa mwanamke wa kidini, mwanamke wa kiroho, mwanadamu aliyekamilika, aliyetimiza sifa zote za ubinaadamu, mwanamke wa kweli na mwanadamu wa kweli. Alikuwa kiumbe wa kiroho ambaye alidhihiri ulimwenguni katika umbile la binaadamu, bali kiumbe wa Mwenyezi Mungu aliyedhihiri katika sura ya mwanamke…..”

Sifa za uchaji-Mungu zilizokuwa katika uepo wa Bibi Fatima Zahra AS, zilipelekea kupendwa sana na Mtukufu Mtume wa Mwenyezi Mungu SWT. Moja ya sifa hizo maalumu alizokuwa nazo mwanamke huyo ni imani na itikadi kamili kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Siku ya Malipo, mambo ambayo yalienea katika mwili wake wote. Mtukufu Mtume anasema: "Binti yangu, Fatimani mtu ambaye Mwenyezi Mungu ameuumba moyo wake kwa imani na yakini.” Tazama kitabu cha Biharul-Anwar juzu ya 43. Kwa hakika nuru ya imani hiyo na itikadi, ni mambo yaliyopatikana kutokana na ibada na dua za dhati kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mtume anazungumzia ibada ya sala ya tahajudi iliyokuwa ikisimamishwa na binti yake huyo kwa kusema: "Fatima ni pambo la mwanadamu, wakati wowote anaposimama katika mihrab mbele ya Mola wake, nuru yake huwaangazia malaika wa mbinguni, mithili ya nuru ya nyota kwa watu wa dunia. Wakati huo Mwenyezi Mungu huwaambia malaika kwamba, enyi malaika wangu! Hebu muangalieni mja wangu Fatimani namna gani alivyosimama mbele yangu huku mwili wake ukiwa unatetemeka kwa kuniogopa! Tazameni ni namna gani moyo wake unavyonielekea mimi! Basi shuhudieni kwamba nimemuepusha yeye na wafuasi wake kutokana na moto.” Mwisho wa kunukuu. Tazama kitabu cha Musnad Fatima-Zahra ukurasa wa 72.

Ni kwa kuzingatia sifa hizo maalumu katika shakhsia ya mwanamke huyo, na kupambika kwake na matukufu ya hali ya juu ya kimaanawi, bila kusahau elimu, uchaji-Mungu ndipo akafahamika kuwa mwanamke mwenye daraja ya juu zaidi kati ya wanawake wote wa dunia, kiasi kwamba, hakuna mwanamke aliyeweza kufikia daraja yake. Imepokewa riwaya nyingine kwamba siku moja Mtume alimwambia Bibi Fatima kwa kusema: "Wewe ni mbora wa wanawake wa dunia. Fatima akasema: Ewe baba! Basi iko wapi nafasi ya Maryam? Mtume akasema: Yeye alikuwa kiongozi wa wanawake wa zama zake na wewe ni kiongozi wa wanawake wote wa ulimwengu.” Mwisho wa riwaya. Aidha imeelezwa kwamba, wakati Mtume alipokuwa katika maradhi ambayo alifia ndani yake, alimwita kwa upole binti yake huyo na kumwambia: ”Ewe Fatwimah! Je hauridhiki kuwa mwanamke bora wa ulimwengu na mwanamke bora wa umma huu na mwanamke bora kati ya waumini.” Mwisho wa kunukuu. Tazama kitabu cha Sahih Bukhari juzu ya 4.

Kama tulivyogusia huko nyuma, daima Mtume Muhammad SAW alikuwa akimuarifisha Bibi Fatima Zahra kwa watu kwa namna iliyo nzuri na wakati mwingine alisikika akisema: "Yeyote anayemtambua mwanamke huyu basi amefahamu. Ama mtu yeyote ambaye hajamfahamu basi afahamu kwamba yeye anatokana na sehemu ya nyama yangu na roho na moyo wangu. Kwa ajili hiyo mtu yeyote atakayemuudhi yeye basi atakuwa ameniudhi mimi.” Mwisho wa riwaya. Aidha imepokewa kwamba, siku moja Mtukufu Mtume aliingia katika nyumba ya binti yake huyo, huku akiwa na mume wake yaani Imam Ali AS na watoto wao wawili ambao ni Hassan na Hussein, wakati huo malaika wa wahyi akashuka na aya ya 33 Suratul-Ahzab inayosema: "…Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume na kukusafisheni barabara.” Mwisho wa aya. Ni kitokana na nafasi hiyo ya kipekee ya watu hao watano, ndipo wakatambuliwa kuwa viumbe bora zaidi duniani na ambao ndio asili ya chimbuko la uongozi hasa kwa kuzingatia kuwa ni watu wasafi waliotakaswa kutokana na kila aina ya machafu. Inaelezwa kuwa, baada ya kushuka aya hiyo, Mtukufu Mtume SAW akiwa ameishika mikono ya Imam Ali na Fatima, alinyanyua uso wake mbinguni na kusema: "Mola wangu! Hawa ni familia yangu na watu wangu wa karibu, nyama yao ni nyama yangu, na damu yao ni damu yangu. Hivyo waondolee uchafu na uwatakase kabisa kabisa.”

3483462

Published: 1
Under Review: 0
non-publishable: 0
abdul shakur mahmoudl
0
0
asante sana mtungaji wa hadithi yenye kusisimua na yenye kufahamika nakupa pongezi sana mimi mwenyewe binasfi nimeipenda sana historia na kama ziko nyengine please. asante
Name:
Email:
* Comment: