IQNA

Utawala wa Kifalme Bahrain wavunja Chama cha Kiislamu cha Al Wifaq

17:57 - July 18, 2016
Habari ID: 3470461
Utawala wa Kifalme Bahrain umekivunja chama cha Kiislamu cha al-Wefaq ambacho ndio chama kikuu cha upinzani nchini humo.

Uamuzi huo umetangazwa na mahakama inayodhibitiwa na ufalme ambapo mbali na kubatilishwa usajili wa chama hicho, mahakama  hiyo imeagiza kuzuiliwa fedha na mali zote zinazomilikiwa na chama hicho chenye idadi kubwa ya wafuasi. Hatua hiyo ya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa imekosolewa vikali na mashirika ya kutetea hazi za binadamu duniani.

Shirika la haki za binadamu la Human Rights First limekosoa hatua ya kupigwa marufuku chama hicho na kusema kuwa huo ni mwendelezo wa wimbi jipya la ukandamizaji wa utawala wa Manama wa kutaka kuvifunga mdomo vyama vya upinzani nchini humo.

Brian Dooley, ofisa wa shirika hilo amesema kuwa, kusimamishwa shughuli za chama kikuu cha upinzani nchini humo kunadhihirisha namna serikali ya Bahrain inavyokusudia kufunga majukwaa na njia zote za wananchi za kujieleza na kutoa malalamiko ya na kwamba, mkondo huo wa kuvinyamazisha vyama vya siasa ni hatari na unaweza kuchochea zaidi mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi. Juni 14 mwaka huu, Wizara ya Sheria ya ukoo wa Aal Khalifa ilitangaza kusimamishwa shughuli zote za chama cha al Wefaq, siku moja baada ya kumkamata Nabeel Rajab, mkuu wa kituo cha haki za binadamu nchini humo.

Hii ni katika hali ambayo, Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa chama hicho cha Kiislamu anazuiliwa na utawala wa Aal Khalifa tangu mwezi Disemba 2014, kwa tuhuma za kupanga mapinduzi dhidi ya serikali ya Manama. 

3515683


captcha