IQNA

Waislamu nchini Uganda wataka Wizara ya Masuala ya Kiislamu

8:43 - July 29, 2016
Habari ID: 3470480
Waislamu nchini Uganda wamemtaka Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo kubuni wizara mpya ya masuala ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, wakizungumza mapema Jumatatu wiki hii wakati walipokutana na Rais Museveni mjini Kampala kwa munasaba wa kuzinduliwa mradi wa Nyumba ya Zakat wa kusambaza Zakat, viongozi wa Waislamu walibainisha ulazima wa kuwepo wizara ya kusimamia masuala yao.

"Wakati umefika kwa Waislamu milioni 10 Uganda kupata wizara ya kushughulikia masuala yao”, amesema Kadhi wa Wilaya ya Kampala Sheikh Idrisa Luswabi.

Pamoja na hayo, wakati wa hotuba yake, Rais Museveni hakugusia ombi hilo la Waislamu kutaka wizara ya kushughulikia masuala yao.

Hajj Majid Bagalaaiwo, Mwenyekiti wa Kamati ya Nyumba ya Zakat pia alimlalamikia Museveni kuhusu idadi ndogo sana ya Waislamu ambao wameteuliwa katika baraza la mawaziri.

Akihutubia kikao hicho, Rais Museveni aliwapongeza Waislamu kutokana na usimamizi wao mzuri wa Zakat kupitia kuanzishwa Nyumba ya Zakat, na kuitaja hatua hiyo kuwa ya kimaendeleo.

Uganda ni mwanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na inakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 39.

3518435

captcha