IQNA

Bahrain yalaaniwa kwa kuidhinisha marufuku ya chama cha al-Wefaq

17:35 - September 23, 2016
Habari ID: 3470576
Shirika moja la kutetea haki za binadamu limelaani vikali hatua ya mahakama ya Bahrain kudhinisha marufuku ya chama kikuu cha upinzani nchini humo, al-Wefaq.

Katika Taarifa, mkuu wa utafiti katika Shirika la Amnesty International, Philip Luther amesema uamuzi wa kuidhinisha upigwaji marufuku al-Wefaq ni ukiukwaji wa wazi wa uhuru wa maoni na kukusanyika na ni jaribio la kukandamiza wakosoaji wa serikali ya Bahrain.

Luther amesema watawala wa nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi  wameshindwa kuwasilisha ushahidi wowote kuwa al- Wefaq si harakati ya  amani. Amesema al-Wefaq imekuwa ikijaribu kuleta mabadiliko Bahrain kutokana na kuongezeka ukandamizaji wa serikali.

Mwezi Juni mahakama moja ya Bahrain iliamuri kufungwa ofisi za al-Wefaq na kasha baada ya mwezi moja kupiga marufuku harakati hiyo ya upinzani kwa tuhuma kuwa inachochea ugaidi.

Halikadhalika mwezi Juni mwaka  utawala wa Bahrain ulimpokonya uraia Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mtajika wa Kishia, hatua ambayo ilikabiliwa na radiamali kali baina ya Mashia na ulimwengu kwa ujumla.

Mwezi Mei Mahakama ya Rufaa ya Bahrain  ilizidisha hukumu ya kifungo cha jela cha miaka minne aliyokuwa amekatiwa Sheikh Ali Salman Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Kitaifa ya al Wefaq hadi miaka tisa.

Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa tangu mwezi Februari mwaka 2011. Wananchi wa Bahrain wanataka marekebisho ya kisiasa, huru, uadilifu, kukomeshwa vitendo vya ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Hata hivyo utawala wa Aal Khalifa siku zote umekuwa ukiwakandamiza raia, kuwaua na kuzuia maandamano yao ya amani.

Hivi karibuni, Nchi 35 wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa zimelaani hatua zinazochukuliwa na serikali ya Bahrain dhidi ya wapinzani nchini humo.

Taarifa iliyotolewa Septemba 15 na nchi 35 wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa imelaani ukandamizaji wa serikali ya Bahrain dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa na imetoa wito wa kufanyika marekebisho ya pande zote ya kisiasa na kurejesha utulivu nchini humo.

Umoja wa Ulaya pia umetoa taarifa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ukieleza wasiwasi wake kuhusu suala la kupokonywa uraia wapinzani wa kisiasa wa serikali ya kifalme ya Bahrain.

Taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya ambayo imeungwa mkono na nchi kadhaa wanachama imeeleza pia wasiwasi wake juu ya hatua ya serikali ya Manama ya kukivunja chama cha upinzani cha al Wefaq, hukumu ya kifungo cha miaka 9 jela dhidi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Sheikh Ali Salman, na kuendelea kutiwa nguvuni watetezi wa haki za binadamu nchini Bahrain. 

3532295


captcha