IQNA

Kinara wa magaidi wa ISIS apewa sumu Iraq, hali yake ni mahututi

19:23 - October 03, 2016
Habari ID: 3470596
Kinara wa magaidi wakufurishaji wa ISIS (Daesh), Ibrahim al Sammarai, maarufu kama Abu Bakr al-Baghdadi, amepewa sumu akiwa pamoja na makamanda wengine wa kundi hilo katili.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iraq Media, duru huko kaskazini magharibi mwa mkoa wa Nineveh zinasema  chakula cha Baghdadi kimewekwa sumu na watu wasiojulikana.

Imeelezwa kuwa, chakula cha mchana alichotayarishiwa yeye na makamanda wake watatu kiliwekwa sumu katika makao yake ya wilaya ya Be'aaj kusini magharibi mwa Nineveh.

Duru za kuaminika zinasema wanne hao wako katika hali mahututi kutokana na sumu hiyo na kwamba wamepelekwa katika eneo lisilojulikana wakiwa chini ya ulinzi mkali. Taarifa zaidi zinasema ISIS imeanzisha oparesheni kali kuwasaka walioweka sumu katika chakula cha kinara huyo wa magaidi wakufurishaji.

Magaidi wa ISIS wamekuwa wakiendesha kampeni ya mauaji ya kinyama nchini Iraq na Syria tokea mwaka 2014. Kundi hilo, ambalo linapata himaya ya baadhi ya nchi za Magharibi na pia baadhi ya madola ya Kiarabu hasa Saudi Arabia, limeteka maeneo kadhaa ya nchi hiyo mbali na kuitangaza miji  ya Raqqah Syria, na Mosul, Iraq kuwa makao makuu yake.

Vikosi vya Iraq na Syria kwa himaya ya wanamgambo waitifaki vimefanikiwa kuyakomboa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yamekaliwa kwa mabavu na magaidi wa ISIS.

3461077


Kishikizo: isis daesh iqna baghdadi iraq
captcha