IQNA

6:20 - October 12, 2016
News ID: 3470608
Tuko katika siku hizi za kuomboleza kuuawa shahidi Imam Hussein AS ambaye ni mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW.

Imam Hussein ni dhihirisho kubwa la ukweli na hakika ambaye nuru ya mwongozo wake inaangaza njia ya vizazi vyote vya mwanadamu. Ni safina ya wongofu inayowafikisha kwenye ufukwe wa salama, saada na ushindi watu walioachwa njiani. Kwa hakika iwapo mwanadamu atawaza vyema ataweza kuona na kudiriki kwenye mtukufu huyu kila sifa bora ya utu.

Tuko kwenye siku hizi za majonzi za kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS.

Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili la Yazid bin Muawiya ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi yeye, watoto, ndugu zake na masahaba zake katika siku kama ya leo.

Imam Ali na Bibi Fatma AS binti ya mtukufu Mtume SAW walijaaliwa kupata mwana wao wa pili kwa jina la Hussin AS. Alipopata habari ya kuzaliwa kwake Mtume alienda kwenye nyumba ya Ali na Fatma AS na kuwataka wamletee mwana huyo ili apate kumuona. Mtoto huyo alifungwa kwenye kitambaa cheupe na kukabidhiwa Mtume SAW ambaye aliadhini kwenye sikio lake la kulia na kusoma ikama kwenye sikio lake la kushoto. Katika siku za kwanza za uzao huo mtukufu, Malaika Jibril aliteremka na kumwambia Mtume: "Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mpe mtoto huyu jina la Hussein." Kwa utaratibu huo mwana huyo wa pili wa Ali na Fatimah AS alipewa jina tukufu la 'Hussein' na Mwenyezi Mungu mwenyewe.

Kwa muda wa zaidi ya miaka sita, Imam Hussein AS aliishi na kulelewa na Mtume Mtukufu SAW. Muamala mzuri wa mahaba pamoja na uzingatiaji mkubwa aliopewa Imam Hussein akiwa angali mtoto na Mtume ulibainisha wazi kwamba angelikuwa mtu muhimu na mashuhuri. Kuhusiana na suala hilo Salman Farsi, mmoja wa masahaba muhimu wa Mtume anasema: "Nilimwona Mtume SAW akiwa amemketisha Hussein AS kwenye miguu yake huku akimbusu na kusema: Wewe ni mkubwa, mwana wa mkubwa, na baba wa wakubwa. Wewe ni Imam, mwana wa Imam, na baba wa Maimamu. Wewe ni hujja wa Mwenyezi Mungu, mwana wa hujja wa Mwenyezi Mungu na baba wa mahujja wa Mwenyezi Mungu, ambao ni watu tisa na wa mwisho wao ni Qaim wao yaani Imam Mahdi AF."

Anas bin Malik pia anasema kuhusiana na suala hili: "Wakati Mtume alipoulizwa ni nani kati ya Ahlul Beit wake anayempenda sana alisema: "Hassan na Hussein. Mara nyingi Mtume Mtukufu SAW alikuwa akiwakumbatia kifuani Hassan na Hussein na kuwabusu." Tunaweza kutambua na kudiriki uhusiano mkubwa wa kimaanawi na wa mbinguni uliokuwepo kati ya Mtume na Hussein katika jumla hii ya Mtume SAW aliposema: "Hussein anatokana na Mimi na mimi ninatokana na Hussein."

Hakuna shaka kuwa moja ya njia bora na zenye mafanikio makubwa zaidi katika mbinu za malezi ni utoaji mifano hai inayoonekana na kuhisika. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Qur'ani Tukufu ikatwambia kwamba Mtume Mtukufu ni mfano bora wa kuigwa na sisi wanadamu. Hii ni kwa sababu sifa na thamani zote bora na kamilifu zinapatikana kwa Mtume huyo na katika maneno na njia yake ya maisha.

Hata kama ni vigumu kubainisha sifa za Imam Hussein AS katika makala fupi kama hii lakini ni wazi kwamba maisha yake yaliyojaa rehema, upendo, karama, ukarimu na utukufu, yalikuwa mfano wa mvua ya rehema iliyonyesha kwenye ardhi kavu ya nyoyo za Waislamu na kuvunja kiu yao huku ikizijaza nyoyo hizo uchangamfu, uhai mpya na harakati. Kwa maneno mengine ni kuwa Imam Hussein AS ni nembo ya fadhila na thamani za kiutu na Kiislamu. Imam Hussein AS alikuwa dhihirisho halisi la ushujaa mbele ya maadui wa Uislamu na nembo ya unyenyekevu na kusalimu amri mbele ya Mwenyezi Mungu. Maisha yake yanabainisha wazi malezi ya kiungu aliyoyapata kutoka kwa Mtume SAW. Mapambano yake dhidi ya dhulma yaliandaa uwanja mzuri wa kuenezwa thamani za maadili na kuondolewa vizuizi vyote vilivyozuia kuimarishwa maadili katika jamii. Katika zama za Imam Hussein AS, watawala wa Bani Umaiyya walikuwa wamefuta kabisa thamani za kimaadili zilizowekwa na Mtume Mtukufu SAW. Jambo hilo lilipelekea jamii ya Kiislamu kuegemea upande wa matamanio na upotovu wa kimaadili. Dhulma na upendeleo ulifanyika waziwazi katika utawala wa Bani Umayya. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Imam akaitaja harakati yake ya kurekebisha hali hiyo kuwa harakati ya kuamrisha mema na kukataza maovu. Kupitia harakati hiyo, Imam alinuia kurekebisha jamii na kuielekeza kwenye fadhila na maadili bora kama alivyofanya babu yake Mtume Muhammad SAW. Kwa maelezo hayo harakati na mapambano ya Imam Hussein AS yalisimama juu ya msingi wa utakasaji nafsi na uimarishaji wa thamani za kiakhlaki katika jamii. Hii ndio maana Imam Hussein AS akasema hivi mwanzoni mwa mapambano yake: "Mimi nimetoka kwa ajili ya kufanya marekebisho katika umma wa babu yangu Muhammad SAW na ninataka kuamrisha mema na kukataza mabaya, na kufanya kama alivyofanya babu yangu Muhammad SAW na baba yangu Ali bin Abi Talib AS." Imam Hussein alifuata misingi miwili muhimu katika harakati zake za kuhuisha na kutekeleza mafundisho halisi ya Uislamu katika jamii. Msingi wa kwanza ulikuwa ni kufuata kikamilifu mafundisho ya Qur'ani Tukufu pamoja na sunna za Mtume SAW na msingi wa pili ulikuwa ni kutii na kufuatwa maagizo ya Imam na kiongozi halisi wa umma wa Kiislamu. Kwa utaratibu huo Imam Hussein AS alikuwa akisisitiza kuwa njia pekee ya kuepuka maangamizi na kufikiwa saada ya milele ni kufuata mafundisho ya Ahlul Beit wa Mtume SAW na kuchukua mafundisho ya Qur'ani Tukufu kutoka kwao.

Kabla ya jambo lolote lile Imam Hussein AS alikuwa mja wa Mwenyezi Mungu ana akithibitisha jambo hilo katika maisha na mienendo yake yote. Alikuwa mkarimu na mwenye huruma sana na akifanya kila aliloweza ili kuwasaidia wenzake na kuwakidhia haja zao. Alikuwa akiwavisha nguo masikini na kuwapa chakula wenye njaa. Akiwalipia madeni wenye kudaiwa, kuwapenda mayatima na kuwasaidia watu dhaifu. Alikuwa akifunga na kumwabudu sana Mwenyezi Mungu na wakati huohuo kuonyesha ushujaa mkubwa katika medani za vita. Kamwe hakukubali kudhalilishwa na hatimaye akafadhilisha mauti kuliko kuishi maisha ya udhalilifu. Alikuwa mkweli, mteteaji mkubwa wa haki na wakati huohuo mvumilivu mkubwa mbele ya masaibu na matatizo.

Tunahitimisha Makala hii kwa kunukuu maneno ya Abdallah Alaili mwanafikra wa Misri kuhusiana na shakhsia ya Imam Hussein AS. Anasema: "Tunakutana katika historia na watu wakubwa ambao kila mmoja ameufanya ulimwengu umzingatie kutokana na sifa au jambo maalumu alilofanya. Utapata mmoja ni mashuhuri katika ushujaa, mwingine katika zuhdi na mwingine katika ukarimu. Lakini adhama na ukubwa wa Imam Hussein AS ni mpana kiasi kwamba kila moja ya sifa zake inabainisha umuhimu wake maalumu wa kihistoria. Ni kana kwamba amekusanya thamani zote za mwanadamu."

3536568

Name:
Email:
* Comment: