IQNA

Serikali ya Nigeria yatakiwa imuachilie huru Sheikh Zakzaky

16:24 - January 02, 2017
Habari ID: 3470775
IQNA-Wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wameitaka serikali ya nchi hiyo kumuachilia huru kiongozi wa harakati hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Wajumbe wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria wametoa taarifa Jumatatu ya leo wakimtaka RaisMuhammadu Buhari wa nchi hiyo kumwachia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, mke wake na wanachama wengine wa harakati hiyo wanaoshikiliwa katika korokoro za nchi hiyo.

Msemaji wa Harakati hiyo, Ibrahim Mussa amemtaka Rais Buhari wa Nigeria kukubali uamuzi wa Mahakama ya Federali ya nchi hiyo na kuchukua hatua zinazotakikana za kumwachia huru Sheikh Zakzaky. Amesema wanachama wa harakati hiyo hawajakiuka sheria yoyote ya nchi na kuongeza kuwa, serikali ya Abuja inapuuza amri ya mahakama.

Vilevile msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amemtaka Rais wa nchi hiyo kuchunguza mauaji yanayofanywa dhidi ya wanachama wa harakati hiyo katika majimbo mbalimbali ya Nigeria.

Mapema mwezi uliopita wa Disemba Jaji Gabriel Kolawole wa Mahakama Kuu ya Nigeria aliiamuru serikali na Nigeria kumwachilia huru bila ya masharti yoyote Sheikh Zakzaky na mke wake katika kipindi cha siku 45 zijazo.

Hukumu ya mahakama hiyo ilisema kuwa, kuendelea kushikiliwa Sheikh Zakzaky gerezani bila ya kufikishwa mahakamani ni kukiuka haki zake zinazosisitizwa katika katiba ya Nigeria na kwamba madai ya serikali kwamba inamshikilia Sheikh Zakzaky gerezani kwa shabaha ya kulinda usalama wake na mkewe, hayawezi kukubalika.

Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake alitiwa mbaroni na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 katika kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria kaskazini mwa jimbo la Kaduna ambapo mamia ya Waislamu waliouawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa katika tukio hilo. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashktaka.

Jeshi hilo lilidai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Allamah Sheikh Ibrahim Zakzaky walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.

Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ni mahututi, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.

3558753

captcha