Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, taarifa iliyochapishwa iliyochapishwa
katika mtandao wa kijamii wa Telegram imesema: "Ofisi ya Maulana Sheikh
Hemedi Jalala imepokea taarifa za msiba wa Ayatullah Hashemi Rafsanjani,
Mwenyekiti wa Majlisi ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu Iran. Mwenyezi
Mungu ailaze roho yake pema."
Ayatullah Ali Akbar Hashemi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuanisha
Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu Iran aliaga dunia leo baada ya umri mrefu wa
jihadi na jitihada zisizo na kikomo kwa ajili ya Uislamu na Mapinduzi ya
Kiislamu.
Ayatullah Hashemi Rafsanjani amepata mshtuko wa moyo leo Jumapili usiku
katika hospitali moja Tehran na madaktari wamejitahidi kumpa matibabu ya haraka
lakini hawakufanikiwa.
Hashemi Rafsanjani, ambaye ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 82,
alijiunga na chuo cha kidini akiwa kijana na kuanza masomo ya kidini hadi
kufikia daraja ya Ijtihad.
Tokea mwaka 1958 alijiunga na mapambano dhidi ya utawala wa kiimla wa Shah ambapo alifungwa jela mara saba na
kuendeleza mapambano hayo hadi wakati wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka
1979.
Ayatullah Rafsanjani alikuwa mwenye azma imara katika harakati ya
Mapambano ya Kiislamu yaliyoongozwa na Imam Khomeini MA.
Kati ya nyadhifa ambazo Ayatullah Rafsanjani aliwahi kushika baada ya
ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran, Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi ya
Kiislamu, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Kaimu Amri
Jeshi Mkuu, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Ulinzi wa Kitaifa na nafasi aliyoishika
hadi kifo chake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa
Kiislamu.