IQNA

Kikao cha nchi za Kiislamu kujadili kadhia ya Waislamu wa Rohingya

17:47 - January 12, 2017
Habari ID: 3470792
IQNA-Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeitisha kikao cha nchi wanachama kujadili mauaji na mateso wanaofanyiwa Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar.

Habari zinasema kuwa, Najib Razak, Waziri Mkuu wa Malaysia ndiye anayetazamiwa kuwa mwenyekiti wa mkutano huo wa OIC unaotazamiwa kufanyika wiki ijayo mjini Kuala Lumpur.

Wawakilishi 56 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushrikiano wa Kiislamu OIC wanatazamiwa kushiriki mkutano huo utakaofanyika Januari 19.

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa unafanya uchunguzi kuhusiana na ukandamizaji na mauaji yanayoripotiwa kufanywa dhidi ya jamii ya walio wachache ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar, ukandamizaji unaofanywa na jeshi la nchi hiyo likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali.

Tangu mwaka 2012 Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na maafisa usalama wa Myanmar wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za ukatili, mauaji na hata kubaka wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo.

Serikali ya Myanmar imekataa kuwapa uraia Waislamu wa jamii ya Rohingya wapatao milioni 1.1 na kuwataja kama wahamiaji haramu kutoka Bangladesh.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu hao ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.
Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya vikosi vya serikali na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.
3561989

captcha