IQNA

Aya za Qur’ani alizosomewa Trump baada ya kuapishwa +Video

1:13 - January 23, 2017
Habari ID: 3470807
IQNA: Baada kuapishwa Donald Trump kama rais wa Marekani, Imamu aliyealikwa katika ibada maalumu alisoma aya za Qur’ani ambazo zilikuwa na ujumbe wa wazi kwa rais huyo na utawala wake.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Imam Muhamed Magid, mkurugenzi wa Jumuiya ya Waislamu ya All Dulles Area, ni mtu mashuhuri mjini Washington na amekosolewa na baadhi ya Waislamu kwa kukubali kushiriki katika ibada hiyo iliyoshirikisha wafuasi wa dini mbali mbali siku ya Jumamosi katika Kanisa Kuu (Cathedral) la Kitaifa la Washington.

Imam Magid alikuwa miongoni mwa viongozi 26 wa kutoka dini mbali mbali walioshiriki na kuongoza maombi hayo ya kwanza kuhudhuriwa na rais Trump na ambayo yamekuwa yakifanyika kila baada ya rais kuapishwa tokea enzi za George Washington.

Awali ilikuwa imepangwa kuwa, Sheikh Magid angeadhini tu lakini aliamua kusoma aya za Qur’ani zenye ujumbe maalumu kwa Trump ambaye amekuwa kiibua matamshi yenye utata na chuki dhidi ya Waislamu na wahamiaji nchini Marekani. Sheikh Magid awali alisoma aya ya 13 ya Surah al Hujarat katika Qur’ani Tukufu ampapo Allah SWT anasema: "Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari”.

Aidha Imam Magid alisoma aya ya 22 ya Surat Ar-Rum ambapo Allah SWT anasema: "Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa wajuzi.”

Rizwan Jaka Mkurugenzi wa Jumuiya ya Waislamu ya All Dulles Area ametoa kauli yake kuhusu sababu ya wao kushiriki katika ibada hiyo ya dini mbali mbali iliyohudhuriwa na rais Trump na kusema: "Baada ya uchaguzi, mengi yamesemwa kuhusu Waislamu, kumeibuliwa maswali kuhusu uzalendo wa Waislamu na hivyo aya hizo zililenga kufikisha ujumbe kuwa sote tunapaswa kuja pamoja hata kama tunahitilafiana kwa rangi au lugha kwani hivyo ndivyo Allah alivyotuumba.”

3461995


Aya za Qur’ani alizosomewa Trump baada ya kuapishwa



captcha