Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo mjini Tehran katika ufunguzi wa
mkutano wa sita wa kimataifa wa kuunga mkono Intifadha ya Palestina
unaofanyika hapa mjini Tehran ambapo sanjari na kusisitizia kuwa,
ukandamizaji wa kutisha dhidi ya taifa la Palestina, kamatakamata ya
kila mara, mauaji na uporaji, kughusubu ardhi za taifa hilo, ujenzi wa
vitongoji vya walowezi na njama kwa ajili ya kubadilisha muundo na
utambulisho wa mji mtukufu wa Quds na Masjidul-Aqsa na maeneo mengine
matukufu ya Kiislamu na Kikristo, kunakofanywa na utawala haramu wa
Israel kupitia uungaji mkono wa kila upande wa Marekani na baadhi ya
madola ya Magharibi, ni mambo ambayo kwa bahati mbaya hayakabiliwi na
radiamali yoyote ya walimwengu.
Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, raia wa Palestina wanajifakharisha kwa
kuona kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu yuko pamoja nao na kwamba
wamekabidhiwa ujumbe mtukufu wa kutetea ardhi hizo tukufu na
Masjidul-Aqsa. Kiongozi Muadhamu amefafanua kuwa, uchunguzi uliofanywa
unaonyesha kwamba, katika historia hakuna taifa lolote duniani ambalo
limewahi kukumbwa na machungu, mateso na hatua za kidhalimu kutoka ndani
na nje ya eneo na kukaliwa kikamilifu kwa mabavu huku raia wake
wakitimuliwa majumbani mwao na kisha kuja kundi jingine kukalia maeneo
yale kama taifa la Palestina na kwamba, suala hilo ni moja ya mambo
ambayo yamechafua na yanaendelea kuchafua kurasa za historia.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu
Mtukufu faili hilo la mateso litafungwa. Amesisitiza kuwa kongamano la
sita la kimataifa kwa ajili ya kuunga mkono Intifadha ya Palestina
linafanyika katika hali ambayo dunia na eneo la Mashariki ya Kati
linakabiliwa na hali mbaya. Amebainisha kwamba katika eneo, kwa muda
wote Iran imekuwa ikifanya juhudi za kuunga mkono taifa la Palestina
katika kupambana na njama za dunia na kutokana na hilo siku hizi eneo
hili limekumbwa na machafuko na migogoro mingi. Amesema, migogoro
iliyopo sasa katika nchi kadhaa za Kiislamu imepelekea kupungua uungaji
mkono kwa suala la Palestina na matukufu ya kuikomboa Quds. Kiongozi
Muadhamu amebainisha kwamba uzingatiaji wa migogoro hiyo unaonyesha
kwamba madola yenye kupenda makubwa, yameanzisha utawala wa Kizayuni
katika eneo hili ili kupitia machafuko makubwa na ya muda mrefu, ziweze
kuzuia uthabiti, usalama na maendeleo ya eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa ajili hiyo amesema kuwa licha ya kuwepo tofauti nyingi baina ya nchi
za Kiislamu, tofauti ambazo baadhi ni za kawaida na zingine
zinazotokana na njama za maadui huku zingine zikiwa zinatokana ma
mughafala, lakini kadhia ya Palestina inatakiwa iwe muhimili wa umoja
baina yao.
3576729