IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Maadui wanailenga Iran kiuchumi

21:20 - March 21, 2017
Habari ID: 3470903
TEHRAN (IQNA) Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema lengo la adui ni kuliwekea mashinikizo ya kiuchumi taifa la Iran na kwamba maadui wanataka kuwafanya wananchi wakate tamaa na kukosa imani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo amehutubia mkusanyiko mkubwa wa watu waliokwenda kuzuru Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Ridha (as) katika mji mtakatifu wa Mash'had akisisitiza kuwa, mwaka mpya wa 1396 Hijria Shamsia ni mwaka muhimu kwa Iran katika upande wa kuwepo haja ya harakati muhimu ya kiuchumi.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa kipaumbele cha kwanza kabisa cha taifa la Iran kwa sasa ni suala la uchumi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, bila ya kuwa na uchumi imara hatuwezi kuwa na izza na amani ya kudumu. Amesisitiza kuwa, kuna ulazima wa kudhamini mambo hayo na kwamba hilo haliwezekani bila ya kuwepo umoja wa kitaifa na mshikamano wa taifa wa Mfumo wa Kiislamu.

Ameongeza kuwa jambo lenye umuhimu mkubwa sana kwa mustakbali wa nchi hii ni uzalishaji wa taifa na uzalishaji wa ndani na kwamba hilo ndilo takwa lake kwa viongozi wa serikali. Amesema kuwa miongoni mwa faida za ustawi wa kiuchumi ni kupatikana nafasi za ajira, kuchanua vipawa, ubunifu wa vijana, kutotumiwa fedha ya kigeni ya taifa, kutumiwa vyema mitaji na harakati kubwa ya uuzaji nje bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.

Ameendelea kueleza njia za ustawi wa uchumi na uzalishaji wa ndani akisema: Uagizaji kutoka nje ya nchi wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini unapaswa kutambuliwa kuwa ni haramu kisheria na kikanuni.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kiulinzi na kijeshi kuwa ni ya kustaajabisha na kuongeza kuwa: Nchi ambayo kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ilikuwa tegemezi kikamilifu katika masuala ya kijeshi kwa nchi za kigeni tena kwa nchi adui kama Marekani, hii leo mafanikio yake yanamstaajabisha adui na kumtia hasira.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, iwapo viongozi wa sekta mbalimbali watashikamana barabara na dini, Mapinduzi na utendaji bora, matatizo yote ya nchi yatatatuliwa na hakuna lolote ltakaloshindikana. Amesema, Iran ni nchi tajiri, na ni kwa sababu hiyo ndiyo maana mabeberu wanaikodolea jicho la tamaa lakini watakufa na kuzikwa na tamaa hiyo.

Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria suala la uchaguzi ujao hapa nchini na kusema: Uchaguzi una umuhimu mkubwa nchini Iran na si uchaguzi wa Rais pekee bali pia chaguzi za Bunge na mabaraza ya miji. Amesisitiza kuwa, uchaguzi ni moja kati ya nguzo mbili za demokrasia ya kidini.

Amesisitiza udharura wa wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi ujao na kusema: Hilo ndilo takwa lake muhimu zaidi.

Ametilia mkazo udharura wa kuheshimu sheria katika zoezi zima la uchaguzi na amezitaka taasisi husika kusimamia vyema zoezi hilo. Amesema, kwa matakwa yake Mwenyezi Mungu maadui hawawezi kufanya lolote. 
3585372



captcha