IQNA

Mwanariadha Mwanamke Mwislamu amuandikia Trump

21:13 - March 23, 2017
Habari ID: 3470905
TEHRAN (IQNA)-Mwanariadha Mwanamke Mwislamu Mmarekani aliyeiwakilisha nchi yake katika Olimpiki amemuandikia barua ya malalamiko Rais Donald Trump wa nchi hiyo.

Barua hiyo imeandikwa na Bi.Ibtihaj Mohammad ambaye alikuwa mwanamichezo wa kwanza mwanamke Mmarekani kushiriki katika michezo ya Olympiki akiwa amevalia Hijabu. Bi.Ibtihaj alishiriki katika michezo ya Olympiki mwaka 2016 nchini Brazil akiwa amevalia Hijabu katika mchezo wa vitara (fencing) na alifanikiwa kupata nishani ya shaba.

Katika barua hiyo ya wazi, amesema aliweza kufanikiwa katika Olimpiki pamoja na kuwa yeye ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika na pia Mwislamu mwenye kuvaa Hijabu sambamba na kushiriki katika mchezo ambao haujulikani na wengi. Anasema alipuuza propaganda na kuonyesha dunia kuwa inawezekana kuwa Mwislamu mwenye kujiheshimu na kuwa Mmarekani. Bi. Ibtihaj amemfahamisha bayana Trump kuwa anaeneza hofu kwa fikra na sera zake zilizo kinyume na alivyokuwa akiitazama Marekani.

Akimhutubu Trump, Bi. Ibtihaj ameandika: "Unaitazama Hijabu ninayoivaa kuwa nembo ya tishio na sababu ya watu kuwa na hofu. Umesema, 'Uislamu unatuchukia'. Si tu kuwa tamko hilo si sahihi bali pia linaibua hofu na chuki kama amabvyo tumeona likisababisha utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu na maeneo yetu ya ibada." Mwanariadha huyo ameendelea kumfahamisha Trump kuwa, "Amri yako ya kuwapiga marufuku watu kutoka nchi zenye Waislamu wengi pamoja na wakimbizi kutoka Syria ni jambo litakalo kuwa na taathira mbaya hata nje ya nchi zilizolengwa."

Huku akiashiria kuwepo Waislamu milioni tatu Marekani, Bi. Ibtihaj anasema Waislamu hao wamechangia katika ustawi wa nchi yao na hata kujiunga na jeshi na kupiga katika vita kwa niaba ya taifa la Marekani. Mwanariadha huyo amemtaka Trump awe mnyenyekevu, mwenye busara na ukarimu ambao rais anastahiki kuwa nao. Bi. Ibtihaj amemaliza barua yake kwa kusema: "Mimi kama mazalendo Mmarekani-Mwafrika na Mwislamu, dini yangu inaniamuru kuwa na matumaini. Ninamini tunaweza kukabiliana na chuki kwa mapenzi." Aidha amesema, Marekani inaweza kupata nguvu kutokana na kuwa Wamarekani wametoka katika dini, rangi, tamaduni na staarabu mbali mbali.

Baada ya ushindi wa Trump na kuapishwa kwake Januari 20 kumeshuhudiwa hujuma dhidi ya Waislamu, misikiti na vituo vya Kiislamu Marekani na pia katika nchi jirani ya Canada.

Mwezi moja baada ya ushindi wa Trump katika uchaguzi wa rais Marekani mnamo Novemba 8 mwaka jana, Shirika la Southern Povert Law Centre (SPLC) lilirekedo vitendo 1,098 vya chuki kote Marekani ambapo idadi kubwa ya waliotekeleza vitendo hivyo walimtaja Trump na nara yake ya Kuifanya Marekani Kuwa na Nguvu Tena (Make America Great Again) au matamshi yake dhidi ya wanawake.

3585486

captcha