Nchi 47 wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa leo Ijumaa zimepiga kura zikiunga mkono rasimu iliyowasilishwa na Umoja wa Ulaya kulaani mateso na mauaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya huko Myanmar na kutaka kuchunguzwa suala hilo. Azimio hilo limesisitiza pia ulazima wa kutumwa ujumbe wa uchunguzi huko Myanmar ambao utachunguza vitendo vya unyanyasaji na bughudha wanayokabiliana nayo Waislamu wa kabila la Rohingya yakiwemo mauaji na kuteswa.
Mkoa wa Rakhine huko kaskazini magharibi mwa Myanmar ni makazi ya Waislamu wa Rohingya zaidi ya milioni moja na tangu mwaka 2012 hadi sasa eneo hilo limekuwa likishuhudia ghasia na vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu. Serikali ya Myanmar pia inajizuia kuwapatia Waislamu hao haki zao za kiraia.
Hadi kufikia sasa mamia ya Waislamu wa Rohingya wameuliwa na makumi ya maelfu ya wengine wamezikimbia nyumba zao kwa kuhofia kupoteza maisha na badala yake wamekimbilia katika nchi jirani. Waislamu wa Rohingya karibu elfu 75 wamekimbilia nchini Bangladesh. Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa Waislamu hao wa Myanmar ni jamii iliyodhulumika zaidi duniani na wamekuwa wahanga wa mateso na unyanyasaji mkubwa.
Wakati huo huo Yanghee Le, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu huko Myanmar ametaka iundwe kamati ya uchunguzi kuhusu ukiukwaji wa haki za Waislamu wa Rohingya nchini humo.
Yanghee Lee, Mjumbe Maalumu (Rapporteur Special) wa UN aliyetumwa kuwatembelea Waislamu wa Rohingya waliokimbilia Bangladesh amesema simulizi alizopewa na wakimbizi hao wa Myanmar ni za kuhuzunisha na zinazoashiria ukubwa wa jinai za kutisha wanazofanyiwa wenzao waliobaki Myanmar.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, wanawake Waislamu wa Rohingya wamemueleza jinsi wenzao walivyobakwa kwa umati na maafisa usalama wa Myanmar, baadhi yao wakichinjwa huku watoto wakitupwa kwenye moto mkali wakiwa hai.
Hivi karibuni pia, Zeid bin Ra’ad al-Hussein Kamishna wa Haki za Binadamu aktika Umoja wa Mataifa amesema vikosi vya usalama Myanmar vimetekeleza mauaji ya umati, ubakaji wa Waislamu kigenge na kuteketezwa vijiji vyao katika kampeni mpya ya ukandamizaji iliyoanza mwezi Okotba mwaka jana .
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu hao ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.
Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.
3462456