IQNA

Askofu Mkuu nchini Nigeria

Kuna tafauti baina ya Uislamu na ugaidi kama ule wa Boko Haram

17:03 - March 26, 2017
Habari ID: 3470908
TEHRAN (IQNA)-Askofu Mkuu wa Nigeria amesisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo kati ya wafuasi wa dini za mbinguni na kusema kuwa, ni muhimu sana kuzitofautisha na dini ya Uislamu fikra za kigaidi kama zile za kundi la Boko Haram.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Nigeria, John Olorunfemi Onaiyekan ameyasema hayo mjini Abuja, katika hotuba aliyoitoa katika mkutano wa 'Theolojia Barani Afrika' na kufafanua kuwa, katika kipindi cha miaka 40 iliyopita amekuwa na mahusiano mema na Waislamu na kwamba mazungumzo pekee ndiyo yanayoweza kubadili mitazamo hasi kuhusu dini ya mbinguni ya Uislamu.

Katika hotuba hiyo, Onaiyekan amesema kuwa, kuna udharura wa kuanzishwa daraja la mawasiliano na Waislamu nchini humo. Sambamba na kusisitiza kuwa, Uislamu hauna uhusiano wa aina yoyote na ugaidi wa genge la Boko Haram amesema kuwa, ni suala muhimu kuutofautisha Uislamu na fikra za makundi yenye kufurutu ada.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Nigeria, sambamba na kuashiria kuwa zaidi ya nusu ya jamii ya Wanigeria inaundwa na Waislamu amesema kuwa, uhusiano na mashauriano na wafuasi wa dini hiyo ni suala la dharura, kwani Nigeria inatoa kipaumbele cha mazungumzo kuwa njia pekee ya kumaliza hitilafu.

Matamshi ya kiongozi huyo wa kiroho nchini Nigeria yanatolewa katika hali ambayo Marakeni na baadhi ya nchi za Magharibi zinafanya njama kubwa zenye lengo la kuchafua sura ya Waislamu ulimwenguni kwa kuihusisha dini ya Uislamu na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na wafuasi wa magenge ya kufurutu ada na hatimaye kutekeleza ubaguzi dhidi ya dini hiyo.

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, watu elfu 20 wamepoteza maisha. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu wa Kiwahabbi usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.

3585602/

captcha