IQNA

Mkristo anayefunza Qur'ani Misri kwa muda wa miaka 50

22:35 - April 21, 2017
Habari ID: 3470944
TEHRAN (IQNA)-Misri hivi sasa iko katika hali ya tahadhari ya juu kufuatia hujuma mbili za kigaidi zilizolenga makanisa ya Wakristo wa Kikhufti katika miji ya Tanta na Alexandria na kuua watu 49 siku chache zilizopita.

Lakini pamoja na kuwepo hofu na wasi wasi, Wamisri wanaendelea na maisha, na Waislamu na Wakristo nchini humo wameungana na kuonyesha mshikamano baada ya ugaidi huo.

Lakini hilo si jambo jipya. Kote Misri kuna habari nyingi za Waislamu na Wakristo kuishi pamoja na maelewano.

Kisa kimoja cha kuvutia ni cha mzee mmoja Mmisri ambaye amekuwa akitoa mchango wake wa maelewano ya Waislamu na Wakristo katika jamii kupitia elimu.

Katika kijiji kimoja mkoani Minya nchini Misri, Ayyad Shaker Hanna, ni mwalimu Mkristo mwenye umri wa miaka 80 na ambaye amekuwa akifunza Qur'ani Tukufu kwa muda wa miaka 50 sasa.

Idadi kubwa ya wanafunzi wake watiifu ambao sasa ni wazazi nao pia wamekuwa wakiwaleta watoto wao awafunze Qur'ani. Ayyad huwafunza watoto masomo yote, si Qur'ani tu. Yeye hutoza ada ndogo sana na iwapo familia haiwezi kujimudu kulipa, basi huwasomesha bila malipo.

Ukiwa katika darasa lake utasikia mara kwa mara akiwaambia wanafunzi wake, "hebu soma nisikie," na hapo mwanafunzi huanza kwa kusoma, " Bismillahir Rahmanir Raheem "yaani Kwa Jina Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema na Mwenye Kurehemu.

Ayyad huwasahihisha wanafunzi wake mara kwa mara wanaposoma Qur'ani na pia huwafahamisha maana ya aya wazisomazo. Darasa zake huanza Jumatatu hadi Ijumaa na annasema hujihisi mpweke wakati wa wikendi kwani hakuna watoto wanaomzunguka.

Anasema wanawahimiza wanafunzi wake kuishi katika jamii kwa mapenzi na kuheshimiana.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa, watu wa Misri wanamuenzi afisa wa polisi mwanamke Mwislamu ambaye alipoteza maisha yake akijijaribu kumzuia gaidi wa kundi la ISIS kuingia katika kanisa la Kikhufti mjini Alexandria. Afisa wa polisi Bi. Nagwa Abdel-Aleem aliyekuwa na umri wa 55 alikuwa analinda lango la kanisa hilo la mjini wakati gaidi aliyekuwa amejifunga mshipi wa bomu alipojaribu kupita katika kituo cha upekuzi. Baada ya kuziwa na Bi. Abdel-Aleem kupita, gaidi huyo alijilipua katika mlango wa kanisa. Bi. Abdel-Aleem ni afisa wa kwanza wa polisi mwanamke kupoteza maisha akiwa kazini nchini Misri.

Kuna Wakristo milioni 10 kati ya watu wote milioni 90 nchini Misri. Mara kwa mara Wakristo wa Misri hukabiliwa na hujuma za kundi la kigaidi la ISIS au waitifaki wake.

3462627

captcha