IQNA

Wakristo Kongo DRC wana hamu kujifunza Qur'ani Tukufu

0:25 - April 28, 2017
Habari ID: 3470955
TEHRAN (IQNA)-Haafidh wa Qur'ani tukufu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema Wakongomani wana hamu na shauku kubwa ya kujifunza Uislamu kiasi kwamba Wakristo wa nchi hiyo wanawapeleka watoto wao madrasa ili wakasomeshwe Qur'ani.

Hassan bin Mussa Yasin, qaari na haafidh wa Qur'ani Tukufu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameyasema hayo leo katika mahojiano na Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA na kuongeza kuwa licha ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa nchi ya Kikristo na haina idadi kubwa ya Waislamu lakini kuna madrasa na vyuo kadhaa nchini humo.

Haafidh huyo wa Qur'ani amefafanua kuwa kuna madrasa na vyuo mbalimbali vya Qur'ani nchini humo ambavyo vinafundisha kuhifadhi, kusoma Qur'ani kwa mtindo wa tajwidi pamoja na tarjumi na tafsiri ya Kitabu hicho cha mbinguni.

Akitoa tathmini yake kuhusu mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kulinganisha na yale yanayofanyika katika nchi zingine, Hassan bin Mussa Yasin amesema, kabla ya mashindano ya Tehran amewahi kushiriki mashindano ya Qur'ani ya Algeria na Bahrain, lakini mashindano ya Qur'ani ya Iran ni mashindano bora zaidi aliyowahi kushiriki kwa sababu yalikuwa na uandaaji na uendeshaji mzuri sana na hayawezi kulinganishwa hata kidogo na mashindano aliyoshiriki katika nchi nyenginezo.

Mashindano ya 34 Kimataifa ya Qur'ani ya Iran yalimalizika Jumatano usiku mjini Tehran huku wawakilishi wa Iran katika vitengo vya hifdhi na qiraa wakishika nafasi za kwanza.

Kauli mbiu ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani nchini Iran mwaka huu ilikuwa ni "Kitabu Kimoja Umma Mmoja" kwa kuzingatia mafundisho ya Qur'ani Tukufu ya umoja baina ya Waislamu. Mashindano hayo ya Qur'ani yalikuwa na washiriki 276 kutoka nchi 83 duniani.

3593689

captcha