IQNA

Iraq yapinga mpango wa Bahrain kumbaidisha Ayatullah Qassim mjini Najaf

17:52 - May 25, 2017
Habari ID: 3470993
TEHRAN (IQNA)- Utawala wa Aal Khalifa ukiungwa mkono na Saudi Arabia na Marekani umepanga kuchukua uamuzi wa kumbaidisha Ayatullah Sheikh Isa Qassim mjini Najaf Iraq lakini wakuu wa Iraq wamepinga pendekezo hilo.

Harakati na chokochoko za vyombo vya mahakama na vya kijeshi vya utawala wa kiimla wa Aal Khalifa dhidi ya Sheikh Isa Qassim zilichukua muelekeo mpya siku ya Jumapili iliyopita baada ya kutangazwa hukumu ya kifungo cha nyumbani cha mwaka mmoja dhidi ya mwanazuoni huyo mwanamapambano na hatimaye askari wa Bahrain na Saudia kulivamia eneo la al-Diraz katika mji mkuu wa Bahrain Manama na kuizingira nyumba ya Sheikh Isa Qassim, yakiwa ni maandalizi ya kutaka kumbaidisha alimu huyo.

Wakati huo huo kanali ya televisheni ya Al- Mayadeen ya Lebanon imetangaza kuwa Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi amelikataa ombi la Bahrain la kutaka Ayatullah Sheikh Isa Qassim apelekwe uhamishoni nchini Iraq.

Sambamba na njama hiyo inayopangwa kutekelezwa nautawala wa Aal Khalifa malalamiko na uungaji mkono wa wananchi wa Bahrain umezidi kupamba moto huku maulamaa wa nchi hiyo wakitangaza jana na leo kuwa siku za maombolezo nchini nzima ikiwa ni kuonyesha mshikamano na uungaji mkono wao kwa Sheikh Isa Qassim.

Watu wasiopungua sita waliuawa, wengine zaidi 200 walijeruhiwa na wengine wapatao 300 walitiwa nguvuni juzi Jumanne katika uvamizi ulioandamana na ufyatuaji risasi uliofanywa na vikosi vya utawala wa Aal Khalifa katika eneo la Al Diraz yaliko makazi ya Sheikh Isa Qassim.

Malalamiko na maandamano ya wananchi wa Bahrain dhidi ya watawala dhalimu wa nchi hiyo yamekuwa yakiendelea tokea tarehe 14 Februari 2011. Tokea mwanzoni mwa maandamano hayo watawala wa ukoo wa Aal Khalifa wamekuwa wakitekeleza mbinu tofauti za kupambana na wapinzani.

3603141

captcha