IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Watawala wa Saudia ni wakali kwa Waislamu, lakini warehemevu kwa Makafiri

11:33 - May 28, 2017
Habari ID: 3470998
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa watawala wa Saudi Arabia ni wakali sana kwa Waislamu lakini wakati huo huo ni warehemevu kwa makafiri.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo katika mahafali ya kimaanawi ya Qur'ani katika siku ya kwanza ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani alasiri ya jana mjini Tehran. Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa, watawala wa Saudi Arabia wanawapatia Wamarekani vitita maalumu vya fedha. Kiongozi Muadhamu aliendelea kwa kuhoji, "Je, utajiri huo ni wa nani?. Utajiri huo ni wa wananchi wa Saudi Arabia na unakabidhiwa makafiri ambao ni maadui wa Waislamu.”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, watawala wajinga wa Saudi Arabia wanadhani wanaweza kupata urafiki wa maadui wa Uislamu kwa kuwapatia pesa na kuwapa misaada. Amesema hakuna urafiki hapo, kwani kama wasemavyo hao Wamarekani maadui, wanawakamua Wasaudia kama ng'ombe anavyokamuliwa maziwa na kisha kumchinja. Kiongozi Muadhamu amesema watawala wa Saudia wanawakandamiza wananchi wao kwa njia hiyo huku wakiwakandamiza watu wa Yemen na Bahrain kwa njia nyinginezo. Amesema hatimaye watawala hao wa ukoo wa Aal Saud wataangamia.

Akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei amesema ni jambo la kusikitisha kuwa leo jamii za Kiislamu zimekumbwa na matatizo kama jamii nyingine zisizokuwa za Kiislamu na kuongeza kuwa sababu ya hilo ni kuwa katika baadhi ya nchi za Waislamu kuna watu wasiostahiki ambao wameshikilia madaraka na mfano ni utawala wa Saudi Arabia. Amesema watawala wa Saudia wamekataa kufuata mafundisho ya Qur’ani na hawaamini haki. Ameongeza kuwa, ili kuwahadaa Waislamu, wafalme wa Saudia huchapisha na kusambaza mamilioni ya nakala za Qur’ani bila malipo.

Akibainisha zaidi kuhusu kashfa za utawala wa kifalme nchini Saudi Arabia, Kiongozi Muadhamu amesema watu hawapaswi kuhadaiwa na dhahiri bandia ya utawala huo wa kifalme kwani uko katika batili na kwa yakini batili itaangamia. Amesema watawala hao wanaweza kubakia madarakani kwa muda; na hilo litategemea namna waumini katika jamii hiyo watakavyochukua hatua. Iwapo watachukua hatua sahihi, utawala huo utaanguka haraka na iwapo hawatachukua hatua basi inaweza kuchukua muda kabla ya utawala huo kuangamia.

3598318

captcha