IQNA

Dunia yalaani Hujuma za kigaidi Tehran

17:19 - June 08, 2017
Habari ID: 3471013
Hujuma za kigaidi za kundi la ISIS mjini Tehran Jumatano zimeendelea kulaania kimataifa.

Jana asubuhi, mashambulio mawili tafauti ya kigaidi yalifanywa leo kwa wakati mmoja katika Haram ya Imam Khomeini (MA) na katika jengo la ofisi la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) .

Wizara ya Mambo ya Ndani imetangaza kuwa, watu 18 wamekufa shahidi katika mashambulio hayo ya leo na wengine 50 wamejeruhiwa.

Aidha magaidi 4 waliohusika katika shambulio la kigaidi katika jengo la ofisi za Bunge waliangamizwa kufuatia operesheni kali ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC.

Aidha katika shambulio la kigaidi kusini mwa Tehran, mtu mmoja aliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya watu watatu waliobeba silaha kuvamia Haram ya Imam Khomeini MA. Mmoja wa wavamizi hao aliuawa na maafisa usalama na mwingine ambaye alikuwa mwanamke alijiripua.

Kundi la kitakfiri na kigaidi la ISIS au Daesh limetangaza kwamba, wanachama wake wamehusika na hujuma hiyo ya kinyama.

Mratibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hapa nchini na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya wamelaani mashambulio ya kigaidi yaliyotokea leo hapa mjini Tehran.

Gary Lewis, mratibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iran ametoa radiamali kuhusiana na mashambulio hayo ya kigaidi kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, ambapo mbali na kutoa mkono wa pole kwa familia za waliouliwa na kujeruhiwa katika mashambulio ya kigaidi ya Tehran amesema: Chimbuko la ugaidi ni chuki, lakini mapenzi na jitihada za kuleta amani hatimaye vitashinda.

Naye Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif, ambapo mbali na kulaani mashambulio hayo ya kigaidi ametangaza mshikamano na kuwa pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi hiki.

Wakati huohuo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekaa kimya kwa muda wa dakika moja kwa heshima ya watu waliouawa katika mashambulio ya kigaidi yaliyotokea leo hapa mjini Tehran. Hayo ni kwa mujibu wa ofisi ya uwakilishi ya Japan katika Umoja wa Mataifa ambayo pia imetuma salamu za rambirambi kwa familia za watu waliouawa na kujeruhiwa katika mashambulio hayo.

Wakati huohuo viongozi wa nchi mbalimbali duniani wameendelea kutuma salamu za mkono wa pole na kulaani mashambulio ya kigaidi yaliyotokea leo hapa mjini Tehran.

Rais Vladimir Putin wa Russia ametuma salamu za rambirambi kwa Rais Hassan Rouhani na kusisitiza kuwa: "Jinai hizi zimeonyesha kwa mara nyengine tena udharura wa kupanuliwa ushirikiano wa kimataifa wa kupambana na ugaidi; na mimi ninalilaani vikali shambulio hili." Rais wa Russia aidha amesisitizia utayari wa nchi yake kushirikiana na mshirika wake Iran katika kupambana na ugaidi.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Ujerumani na Italia pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa nao pia wametoa tamko la kulaani mashambulio ya kigaidi yaliyotokea leo hapa nchini. Kituo cha Kiislamu cha London, Uingereza nacho pia kimetoa taarifa kulani hujuma hiyo ya kigaidi.

3607561

captcha