IQNA

Hujuma ya kigaidi Msikitini London na ubaguzi wa serikali, vyombo vya habari

22:38 - June 19, 2017
Habari ID: 3471026
TEHRAN (IQNA)-Mwislamu ameuawa Jumatatu usiku baada ya gaidi kuhujumu Msikiti mjini London Uingereza huku Waislamu wakikosoa vyombo vya habari na serikali kwa ubaguzi baada ya tukio.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, hujuma hiyo, ambayo pia imepelekea watu kadhaa kujurihiwa, ilijiri Jumatatu usiku wakati Waislamu walipokuwa wakiondoka msikitini baada ya kumalizika Sala ya Tarawih katika msikiti eneo la Finsbury Park, kaskazini mwa London. Gaidi alitekeleza hujuma hiyo kwa kutumia gari ambapo aliwagonga kwa makusudi Waislamu waliokuwa wakitoka msikitini huku akipiga mayowe na kusema, "Nitawaua Waislamu Wote.”

Polisi London wamemkamata gaidi aliyetekeleza hujuma hiyo ambaye ametambuliwa kwa jina la Darren Osborne na tayari ameshafunguliwa mashtaka ya ugaidi na mauaji.

Baraza la Waislamu Uingereza limetoa taarifa ya kulaani hujuma hiyo na kuongeza kuwa mtendaji wake alichochewa na "hisia za chuki dhidi ya Uislamu". Waziri Mkuu Theresa May pia amelaani shambulio hilo na kuwapongeza Waislamu waliomkamata gaidi huyo na kumkabidi vyombo vya usalama. Imam wa msikiti uliolengwa, Sheikh Mohammad Mahmoud aliwazuia watu waliokuwa na hasira kumpiga gaidi huyo hadi polisi walipofika eneo la tukio.

Waislamu walalmikia msimamo wa vyombo vya habari, serikali

Wakati huo huo, serikali na vyombo vya habari vimekosolewa kwa kutoonyesha ukali baada ya hujuma ya kigaidi msikitini ikilinganishwa na hali ilivyokuwa baada ya hujuma mbili zingine mbili za kigaidi mijini London hivi karibuni. Polisi hawakutangaza haraka kuwa hujuma dhidi ya Msikiti wa Finsbury Park kuwa ni hujuma ya kigaidi. Katika ripoti za awali Polisi ya London ilisema ‘gari limegongana na wapiti njia’ katika hali ambayo walioshuhudia waliwajulisha maafisa wa usalama kuwa aliyetekekeza hujuma hiyo alikuwa anatangaza wazi kuwa anataka kuwaua Waislamu.

Aidha Waislamu wamekosoa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, kwa kuchukua muda mrefu kabla ya kutangaza tukio hilo kuwa hujuma ya kigaidi iliyotekelezwa na mzungu. Hii ni katika hali ambayo katika hujuma zingine, vyombo vya habari hucharuka na kusema mshambuliaji ni Muislamu aliyetekeleza hujuma kwa jina la Uislamu. Pamoja na kuwa gaidi aliyetekeleza hujuma London ni Mkristo lakini vyombo vya habari wala serikali haijazungumza kuhusu ugaidi wa Kikristo. Hii ni katika hali ambayo kila wakati mtu mwenye jina la Kiislamu au Kiarabu anapotekeleza shambulizi serikali na vyombo vya habari hutangaza mara moja kuwa tukio ni ‘ugaidi wa Kiislamu.’

Msikiti wa Finsbury umetoa taarifa na kulaani shambulio hilo na kusema: "Tumesikitishwa sana na vyombo vikuu vya habari kwa kutotangaza mara moja kuwa tukio hili ni hujuma ya kigaidi katika hali ambayo kwa kawaida katika mashambulizi mengine ambayo wahusika hudai kuwa ni Waislamu, vyombo vya habari husema ugaidi huo huwa umetekelezwa kwa jina la Uislamu.”

3611292

captcha