IQNA

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq

Kinara wa kundi la kigaidi la ISIS/Daesh, al Baghdadi, yungali hai

9:17 - July 17, 2017
Habari ID: 3471070
TEHRAN (IQNA)-Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq imekanusha habari za kuangamizwa kinara wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh Abu Bakar al Baghdadi na kusema yungali hai mafichoni nchini Syria.

Mtandao wa habari wa Furat News wa nchini Iraq, umemnukuu mkuu wa kitengo cha taarifa na vita dhidi ya ugaidi cha Wizara ya Mambo ya Ndani ya ya Iraq, Abu Ali al Basary akisema kuwa, kwa mujibu wa taarifa walizo nazo kutoka katika mashirika ya kijasusi ya Kiarabu na kimataifa, Abu Bakar al Baghdadi, mkuu wa genge la kigaidi la Daesh bado yuko hai na amejificha nje ya mji wa Raqah wa kaskazini mwa Syria.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq ametahadharisha kuwa, kufurushwa magaidi wa Daesh na kukombolewa mji wa Mosul hakuna maana ya kumalizika vitendo vya kigadi kwani magaidi wanahatarisha usalama wa nchi zote za eneo hili.

Mkuu wa kitengo hicho cha kupambana na ugaidi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq amesema ushahidi wa hayo ni kuripotiwa mashambulio ya magaidi wa Daesh katika miji mbalimbali duniani hata baada ya kufurushwa mjini Mosul na kupata pigo kubwa katika nchi mbili za Iraq na Syria.

3619428

Amesema, Daesh imetuma magaidi katika nchi mbalimbali kupitia Uturuki ili kueneza hofu na mashambulizi ya kigaidi katika kona tofauti duniani.

Baada ya kukombolewa kikamilifu mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa wa kaskazini mwa Iraq, genge la kigaidi la ISIS lilitoa taarifa tarehe 11 mwezi huu wa Julai na kuthibitisha habari za kuuawa kiongozi wake, Abu Bakar al Baghdadi.

Katika taarifa yake hiyo fupi, kundi la Daesh lilidai kuwa litamteua mtu mwiingine wa kushika nafasi ya Abu Bakar al Baghdadi.  


Kishikizo: iqna isis au daesh
captcha