IQNA

Indhari ya Interpol

Magaidi Sugu wa ISIS wapatao 173 wanahatarisha usalama wa Ulaya

14:13 - July 22, 2017
Habari ID: 3471078
TEHRAN (IQNA)-Polisi ya Kimataifa (Interpo) imechapisha orodha ya wanachama 173 wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh wanaohatarisha usalama wa nchi za Ulaya.

Katika taarifa Interpol imesema magaidi hao wa ISIS wamepata mafunzo ya kutekeleza hujuma za kujiangamiza barani Ulaya kama njia ya kulipiza kisasi kufuatia pigo ambalo kundi hilo limepata katika eneo la Asia Magharibi hasa Iraq na Syria.

Vikosi vya kupambana na ugaidi Ulaya vina wasi wasi kuwa baada ya kuangamia khilafa ya bandia ya ISIS huko Iraq na Syria, kuna hatari ya magaidi kujilipua katika maeneo mbali mbali Ulaya.

Interpol imesema haina ushahidi iwapo walio katika orodha hiyo wameingia Ulaya na kwamba inataraji mashirika ya kijasusi barani humo yatachukua hatua za kukabiliana na tishio hilo.

Orodha hiyo ambayo ilisambawza Mei 27 inawataja magaidi wa ISIS kuwa watu ambao, 'yamkini wamepata mafunzo ya kuunda na kutega mabomu kwa lengo la kusababisha vifo. Inaaminika kuwa wanaweza kusafiri kimataifa na kushiriki katika harakati za kigaidi."

Mwezi Mei Mashirika ya kijasusi ya Uingereza yalionya kuwa raia 350 wa nchi hiyo ambao ni magaidi wanachama wa kundi la kigaidi la ISIS wamerejea nchini humo kutoka Syria na sasa ni tishio kubwa kwa usalama.

Maafisa wa usalama wanasema magaidi hao sugu ambao waliondoka Uingereza na kujiunga na kundi hilo la wakufurishaji wamekuwa wakitarajiwa kurejea nyumbani kwani ISIS imekuwa ikipata pigo Syria na Iraq na hivyo kupoteza ardhi ambazo ilikuwa imezikalia kwa mabavu.

Mashirika ya usalama Uingereza yanasema ni vigumu kufuatilia kila gaidi aliyerejea kwani idadi yao ni kubwa na wanarejea kwa mpigo.

Serikali ya Uingereza inasema raia 800 wa nchi hiyo wako nchini Syria na Iraq ambako wamejiunga na kundi la kigaidi la ISIS na wanahesabiwa kuwa tishio kwa usalama wanaporejea makwao.

Mwezi Februari, Polisi ya Ulaya, Europol, ilitangaza kuwa magaidi 5,000 wa ISIS sasa wako Ulaya na kwamba kwa ujumla kuna magaidi 30,000 kutoka nchi 100 duniani ambao wamesafiri Syria na Iraq tokea mwaka 2011 na kujiunga ma makundi ya kigaidi nchini humo.

captcha