IQNA

Masuala ya hitilafu za kimadhehebu yasiibuliwe katika Ibada ya Hija

1:06 - July 26, 2017
Habari ID: 3471087
TEHRAN (IQNA)-Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Jijja ametoa wito kwa Waislamu wasiibue masuala ya hitilafu za kimadhehebu katika Ibada ya Hija.

Akizungumza katika hadhara ya Maulamaa Jumapili mjini Tehran, Hujjatul Islam Sayyed Ali Qadhi Askar amesema, "Sisi tunahimiza umoja wa Umma wa Waislamu duniani na kwa msingi huo masuala yanayovuruga umoja wa Kiislamu yanapaswa kuepukwa.”

Kwingineko katika hotuba yake, Sheikh Qadhi Askar alisema wawakilishi wa Iran katika masuala ya Jija wako nchini Saudi Arabia kuandaa mazingira ya kuwapokea mahujaji Wairani. Inatazamiwa kuwa, mahujaji 85,000 Wairani watashiriki katika ibada ya Hija mwaka huu.

Mwezi Machi mwaka huu Iran ilitangaza kuwa mahujaji wake watashiriki katika Ibada ya Hija mwaka huu baada ya kuzuiwa na Saudia kutekeleza ibada hiyo mwaka jana kutokana na kuvurugika uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi mbili.

Itakumbukwa kuwa, mnamo Septemba 2015, kulijiri msongamano mkubwa wakati wa ibada ya Hija katika eneo la Mina karibu na Makka ambapo duru zisizo rasmi zinasema Mahujaji 7,000 walipoteza maisha huku Saudia ikisisitiza ni watu 770 waliouawa katika msongamano huo. Iran ilitangaza kuwa mahujaji wake wapatao 465 walipoteza maisha katika maafa hayo ya Mina. Siku kadhaa kabla ya tukio hilo, Mahujaji 100 walipoteza maisha katika Msikiti Mtakatifu wa Makka, wakiwemo Wairani 11 baada ya winchi kuwaangukia wakati wanapotufu.

Miongoni mwa masharti ya kuanza tena safari za Hija kwa Waislamu wa Iran ni kudhaminiwa haki zinazohusiana na masuala ya viza, udharura wa serikali ya Saudi Arabia kutoa dia ya mahujaji walioaga dunia katika eneo la Mina, kulindwa heshima na utukufu wa mahujaji na vilevile kudhaminiwa usalama na utulivu wakati wa ibada ya Hija.

3622079

captcha