IQNA

Mtoto wa miaka 6 Nigeria ahifadhi Qur’ani kwa mwaka moja

10:57 - August 06, 2017
Habari ID: 3471107
TEHRAN (IQNA)-Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka sita nchini Nigeria amewashangaza wengi kwa kufanikiwa kuhifadhi Qur’ani Tukufu kikamilifu kwa kipindi cha chiniya mwaka moja.

Kwa mujibu wa mwandishiw wa IQNA, Salim Abdulkarim, ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Kimataifa ya Profesa Ango Abdullahi katika mji wa Zaria, jimbo la Kaduna kaskazini mwa Nigeria, alianza kuhifadhi Qur’ani Mei 2016 na kufanikiwa kuhifadhi kikamilifu kitabu hicho kitakatifu kabla ya Mei 2017.

Akizungumza na waandishi habari Salim alisema: "Nataka kuwa daktari na lengo langu kuu ni kutoa mchango katika ustawi na maendeleo ya nchi yangu, Nigeria. Iwapo ndoto yangu itatimia, nitawasaidia watu wagonjwa. Naamini kuwa kwa bidiI na motisha kutoka kwa walimu na wazazi wangu, nitafanikiwa kuwa daktari.”

Kwa upande wake, afisa msimamizi wa shule hiyo Malam Hamza Jibril anasema: "Salim aliletwa shuleni hapa na wazazi wake Mei 2016. Baba yake ni Profesa Abdulkarim S. Ahmed ambaye ni mhadhiri wa Uhandisi wa Kemikali katika Chuo Kikuu cha Ahmadu Bello mjini Zaria. Wakati Salim alipofika shuleni alikuwa hajui hata herufi za kiarabu na hivyo hakuwa na uwezo wa kusoma Qur’ani Tukufu. Kwa hivyo tulianza kutoka mwanzo.”

Malam Jibril alisema kutokana na uwezo mkubwa alionao Salim, atashiriki katika mashindano ya Qur’ani nchini Saudi Arabia.

Baba yake Salim amebainisha furaha yake kutokana na mafanikio aliopata mwanae kwa kusema: "Tunapaswa kukumbuka kuwa jukumu la kuwalea watoto liko mikononi mwa wazazi na hivyo tunapaswa kulipa uzito mkubwa suala hilo. Tunapaswa kujaribu kadiri ya uwezo wetu kuwahimiza watoto wetu kuhifadhi Qur’ani Tukufu na kuhakikisha wanapata maarifa ya Kiislamu.”

3463558/

captcha