IQNA

Chuo Kikuu cha Al-Mustafa kusajili washiriki wa Olimpiadi ya Qur’ani, Hadithi

11:21 - September 19, 2017
Habari ID: 3471181
TEHRAN (IQNA)-Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa SAW kimetangaza kuanza kusajili majina ya wanachuo wa kigeni nchini Iran watakaoshiriki katika Olimpiadi ya 23 ya Kimataifa ya Qur’ani na Hadithi.

Kwa mujibu wa taarifa ya chuo kikuu hicho, usajili utaendelea hadi Oktoba 9. Katika kategoria ya kwanza wanachuo watashindana katika Tafsiri ya Qur’ani, Hadithi na Nahjul Balagha. Aidha kutakuwa na kategoria ya kusoma Qur’ani Tukufu (Tahqiq na Tarteel), kuhifadhi Qur’ani na kuhifadhi Nahjul Balagha.

Olimpiadi hiyo ya wanachuo wa kigeni katika vyuo vikuu vya kidini Iran inalenga kubaini vipaji vya wanachuo wa kigeni katika uga wa Qur’ani na Hadithi na pia kuimarisha umoja baina ya wafuasi wa madhehebu mbali mbali za Kiislamu.

Chuo Kikuu cha Al Mustafa kina makao yake katika mji mtakatifu wa Qum ulio kusini mwa Tehran na pia chuo hicho kina matawi kadhaa duniani ambapo wanafunzi husoma Uislamu na taaluma husika.

Chuo hicho kinatoa shahada ya kwanza, shahda ya uzamili na shahada ya uzamifu katika taaluma kama vile fiqhi, theolojia, historia ya Uislamu, uchumi wa Kiislamu n.k. Maelezo zaidi yanapatikana katika tovuti ya chuo ambayo ni http://en.miu.ac.ir/

3643548

captcha