IQNA

Jaribio la kuwazuia Waislamu kuswali Ijumaa mjini Paris

19:28 - November 11, 2017
Habari ID: 3471258
TEHRAN (IQNA)-Tafrani iliibuka Ijumaa katika kitongoji kimoja cha mji mkuu wa Ufaransa Paris, baada ya baadhi ya wakazi wa mji kujaribu kuwazuia Waislamu kuswali Sala ya Ijumaa.
Jaribio la kuwazuia Waislamu kuswali Ijumaa mjini ParisKwa mujibu wa taarifa, tukio hilo limejiri katika kitongoji cha Clichy-la-Garenne wakati watu karibu 100 wenye chuki dhidi ya Waislamu, wakiongozwa na meya wa kitongoji hicho Remi Muzeau, walipojaribu kuwazuia Waislamu kuswali katika barabara iliyo katika eneo la soko la mji. Watu hao waliokuwa wamebeba bango lililokuwa limeandikwa "Sitisheni Sala Barabarani, ni Kinyume cha Sheria". Waislamu katika eneo hilo wamekuwa wakiswali Ijumaa katika barabara kwa miezi kadhaa sasa kulalamikia hatua ya manispaa kufunga chumba cha kuswali walichokuwa wametengewa katika eneo hilo.

Pamoja na kuwepo bughudha hiyo, Waislamu walifanikiwa kuswali Sala ya Ijumaa pembeni mwa barabara ingawa wengi walilazimika kukimbia eneo hilo kwa kuhofia kuhujumiwa.

Huku Waislamu wakitamka Takbir, watu waliokuwa wakiwapinga nao walisikika wakiimba wimbo wa taifa wa Ufaransa na wengine walionekana wakiwa wamebeba misalaba.

Watu hao wenye chuki dhidi ya Waislamu walipasua bango lililokuwa limeandikwa: "Muungano kwa Ajili ya Msikiti wa Jamia wa Clichy." Polisi walilazimika kutenganisha makundi hayo mawili ili kuepusha ghasia zaidi. Hatahivyo kuna wasiwasi wa kuibuka machafuko kwani meya wa Muzeau ameahidi kurejea tena Ijumaa ijayo kuwazuia Waislamu kuswali huku akisema ikiwezekana watakuwa wanafika hapo kila Ijumaa.

Sheikh Hamid Kazed, mwenyekiti wa Muungano wa Jumuiya za Waislamu katika kitongoji cha Clichy ambaye alisalisha Ijumaa amesema wataendelea kuswali katika eneo hilo hadi pale patakapofanyika mazungumzo ya kuwatafutia Waislamu sehemu mbadala ya kuswali.

Uislamu ni dini ya pili kwa ukubwa Ufaransa huku ikikadiriwa kuwa kuna Waislamu milioni tano nchini humo. Waislamu katika miji mingi wanalazimika kuswali barabarani kutokana na kukosekana maeneo ya kuswali au kukosekana nafasi za kutosha ndani ya misikiti jambo ambalo limeibua hisia za chuki dhidi ya Waislamu nchini humo.

Waislamu wa Clichy wamekuwa wakikodi ukumbi wa sala unaomilikiwa na manispaa lakini meya wa eneo hilo aliamia kugeuza ukumbi huo kuwa maktaba na hivyo Waislamu wakazuiwa kuswali eneo hilo.

Manispaa ya Clichy inawataka Waislamu waswali katika kituo kipya cha Kiislamu lakini Waislamu wanasema kiko mbali sana na pia hakuna nafasi ya kutosha kuswali Ijumaa.

3464389

captcha