IQNA

Waislamu 7 wauawa katika machafuko Jamhuri ya Afrika ya Kati

15:29 - November 14, 2017
Habari ID: 3471263
TEHRAN (IQNA)- Waislamu 7 wameuawa na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa katika hujuma dhidi yao mjini Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Henri Wanzet Linguissara, amesema kuwa, watu wawili waliokuwa wamepanda pikipiki walikwenda karibu na mkusanyiko wa watu waliokuwa katika magahawa Jumapili usiku kwa lengo la kuhimiza maelewano na amani nchini humo na kurusha guruneti katikati ya kundi la watu. Mgahawa huo uko karibu na eneo la PK5 ambalo wakaazi wake wengi ni Waislamu.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Simplice Mathieu Sarandji, amewataka wananchi wa nchi hiyo kuwa watulivu na kujiepusha na machafuko. Mapigano makali ya kutumia silaha yalitokea katika eneo lenye Waislamu wengi baada ya shambulio hilo.

Mashambulizi hayo yametokea huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitarajiwa kulipigia kura azimio lililopendekezwa na Ufaransa kuhusu kutumwa wanajeshi 900 wa ziada kwa ajili ya kuwalinda raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wiki hii. Mwaka 2013 mji wa Bangui ulikumbwa na machafuko mabaya ya kidini baina ya Waislamu na Wakristo na tangu wakati huo hadi hivi sasa hali haijarejesha katika mazingira yake ya kawaida.

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo,François Bozizé. Baada ya rais Mwislamu, Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi na magaidi wa Kikristo wenye kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.

Djotidia alilazimishwa na nchi za kieneo kujiuzulu Januari mwaka 2014 na hapo mauaji ya Waislamu yakashika kasi zaidi. Kabla ya kuanza mgogoro, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, ulikuwa na wakaazi 130,000 Waislamu lakini sasa taarifa zinasema idadi hiyo ni chini ya 1,000.

Aidha watu zaidi ya 400,000, wengi wakiwa ni Waislamu wamelazimika kukimbia makazi yao huku wengine milioni 2.7, au nusu ya watu wote CAR wanahitaji msaada. Mauaji ya Waislamu CAR yanajiri pamoja na kuwepo vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini humo.

3663178

captcha