IQNA

Mashindano ya Qur’ani, Hadithi Algeria kwa Munasaba wa Maulidi ya Mtume SAW

12:49 - November 24, 2017
Habari ID: 3471275
TEHRAN (IQNA)-Mashindano kadhaa ya Qur’ani na Hadithi yanafanyika kote Algeria kwa munasaba wa Maulidi ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad al Mustafa SAW.

Kwa mujibu wa taarifa, mashindano hayo yameandaliwa na Idara ya Wakfu na Masuala ya Kidini katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Afisa wa idara hiyo, Sayyid Zuhair Buzare, amesema tayari mashindano hayo yameshaanza katika misikiti kadhaa ya mji mkuu, Algiers na kuongeza kuwa, lengo la mashindano hayo ni kustawisha uwezo wa kuhifadhi Qur’ani Tukufu na Hadithi za Mtume SAW.

Aidha amesema washindi watatunukiwa zawadi katika sherehe itakayofanyika katika Msikiti wa Jamia wa Algiers kwa munasaba wa Siku Kuu ya Maulidi ya Mtume SAW.

Sayyid Buzare amebainisha kuwa mashindano hayo yatakuwa na kategoria sita katika vitengo viwili vya wanawake na wanaume.

Kuhusiana na Maulidi au kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia. Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Kishia linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo.

3666157

captcha