IQNA

Waislamu 305 wauawa baada ya magaidi wa Kiwahhabi kuhujumu msikiti wa Twariqa Misri

21:12 - November 24, 2017
Habari ID: 3471278
TEHRAN (IQNA)- Waislamu wasiopungua 305 wameuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika shambulizi la magaidi wa Kiwahhabi dhidi ya msikiti mmoja wa Twariqa katika Peninsula ya Sinai nchini Misri.

Duru za polisi nchini humo zimesema genge la kigaidi limeushambulia Msikiti waal-Rawdhah ulioko katika mji waBir al-Abd, yapata kilomita 40 kutoka mji wa AL-Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini.

Habari zinasema kuwa, magaidi hao waliokuwa wamejizatiti kwa silaha wameshambulia kwa bomu msikiti huo, na kisha kuanza kuwafytulia risasi ovyo waumini wa Kiislamu waliokuwa wanashiriki hotuba na Sala ya Ijumaa katika msikiti huo.

Baadhi ya mashuhuda wamesema kuwa, magaidi hao wamemeonekana wakizifyatulia risasi pia ambulensi zilizokuja kuwabeba majeruhi wa hujuma hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Misri amesema watu wasiopungua 80 wamejeruhiwa katika shambulio hilo kinyama.

Rais Abdulfattah al-Sisi wa Misri sanjari na kulaani hujuma hiyo, ameitisha mkutano wa dharura na vyombo vya usalama huku akitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa, kufuatia ukatili huo wa magaidi.

Msikiti huo umelengwa kutokana na kuwa aghalabu ya wanaoswali hapo ni Waislamu Kisuni wenye itikadi za Twariqa au Kisufi ambazo hupingwa vikali na Mawahhabi wakufurishaji.

Msikiti wa al-Rawdhah uko katika eneo alimozaliwa Sheikh Eid al-Jariri, mwanazuoni wa Kiislamu anayetambuliwa kama mwanzilishi wa itikadi za Kisufi katika Rasi ya Sinai nchini Misri.

Hadi sasa hakuna kundi lililodai kutekeleza shambulizi hilo linalotajwa kubwa zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu, tangu vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika vianze kukabiliana na magenge ya kigaidi na kitakfiri.

Eneo hilo la kaskazini mwa Misri limekuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye silaha yenye mafungamano na kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS tangu mwaka 2013.

3666463

captcha