IQNA

Waislamu zaidi ya Milioni moja Warohingya wako katika kambi za wakimbizi Bangladesh

20:09 - January 19, 2018
Habari ID: 3471360
IQNA (TEHRAN)-Serikali ya Bangladesh inasema wakimbizi Waislamu Warohingya waliopata hifadhi nchini kufuatia ukatili wanaotendewa nchini Myanmar sasa wamefika milioni moja na idadi hiyo ni kubwa zaidi ya ile ambayo imekuwa ikitajwa katika vyombo vya habari.

Jeshi la Bangladesh limetumia mbinu ya usajili wa mfumo wa kidijitali ujulikanao kama biometric kuwahesabu wakimbizi hao na sasa imebainika idadi ya Waislamu Warohingya walioingia nchini humo kutoka Myanmar imepindukia milioni moja.

 "Hadi sasa tumewasajili Warohingya 1,004,742 na tumewapa kadi za kibimetric," amesema  Brigedia Jenerali Saidur Rahman wa Jeshi la Bangladesh ambaye anasimamia mradi huo wa kuwasajili wakimbizi Warohingya. Anasema kuna maelfu ya wakimbizi wengine ambao bado hawajahesabiwa. Idadi hiyo ni zaidi ya ile ambayo imekuwa ikitajwa na Umoja wa Mataifa ambayo ni 962,000 na inayowajumuisha Warohingya wote wanaoishi Bangladesh wakiwemo 655,000 walioingia nchini humo tokea Agosti 25 mwaka jana wakati Jeshi la Myanmar lilipoanzisha wimbi jipya la mauaji ya kimbari ya Waislamu katika jimbo la Rakhine. Taarifa zinasema  Waislamu wapatao 6,700 waliuawa katika muda wa mwezi moja wakati wanajeshi na Mabuddha wenye misimamo mikali walipoanzisha kampeni ya mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu.

Wakati huo huo, mamia ya wakimbizi wa Kirohingya walioko nchini Bangladesh leo Ijumaa wamefanya maandamano wakipinga mpango wa kuwarejesha nchini Myanmar, ambako walikimbia mauaji na mashambulizi kutoka kwa jeshi la nchi hiyo likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema hali katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar sio shwari kuweza kuwapokea malaki ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbilia nchini Bangladesh. Serikali ya Bangladesh inasema imefikia mapatano na Myanmar kuwarejesha Waislamu waliokimbilia nchini humo.

Zeid Ra’ad Zeid al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani jinai na ukatili unaofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na kusisitiza kuwa, huo ni mfano wa wazi wa kuangamiza kizazi na kaumu ya watu wa jamii fulani.

/3464980

 

captcha