IQNA

Maelfu ya Waislamu China wapelekwa kambini kufunzwa Ukomunisiti kwa lazima

23:19 - January 27, 2018
Habari ID: 3471373
TEHRAN (IQNA)-Waislamu zaidi ya 100,000 kutoka jamii ya Uighur nchini China wanasemekana kushikiliwa kwa nguvu katika kambi zenye msongamano mkubwa ambapo wanafunzwa itikadi za Kikomunisti.

Kambi hizo-ambazo zinashabihiana na kambi za kulazimisha kufanya kazi za  laogai za zama za Mao-zinashikilia karibu Waislamu 120,000 katika eneo la Kahgar katika jimbo la Xinjiang kaskazini magharibi mwa China.

Idadi ya Waislamu wanaoshikiliwa imetolewa na afisa mmoja wa usalama hapo Kashgar ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Kambi hizo ambazo zimepewa jina la 'kambi za kuelimisha upya' zilianza kujazwa Waislamu wakati wa Kongamano la 19 la Chama cha Kikomunisti China Oktoba mwaka 2017. Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, wanaoshikiliwa hapo wanatazamwa kama watu wenye misimamo iliyotajw akuwa 'mikali' ya kidini au mitazamo 'isiyo sahihi ya kisiasa'. Watetezi wa haki za binadamu wanasema kwa mtazamo wa wakuu wa utawala wa Kikomunisti  China, 'misimamo mikali' ni pamoja na kuswali sala tano.

Wakuu wa China wanadai kuwa kambi hizo ni shule za 'kukabiliana na misimamo mikali', kufunza lugha ya Kichina na kutoa mafunzo kuhusu sharia za China zinazohusu Uislamu.

Mkoa wa Xinjiang una wakazi Waisalmu zaidi ya milioni 10 kutoka kabila la Uighur na katika miaka ya hivi karibuni eneo hilo limeshuhudia makabiliano makali baina ya wanajeshi na Waislamu.

Serikali ya China imechukua hatua kadhaa kuwadhibiti Waislamu katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kumteuwa Mkomunisti mwenye misimamo mikali Chen Quanguo kuwa katibu wa chama tawi la Xinjiang tokea mwaka 2016.

3465045/

captcha