IQNA

Chuo Kikuu cha Qur'ani Kujengwa Malaysia

15:29 - April 09, 2018
Habari ID: 3471459
TEHRAN (IQNA)-Chama cha Barisan Nasional nchini Malaysia kimetangaza mpango wa kujenga Chuo Kikuu cha Qur'ani nchini humo ambapo watakaohitimu hapo watakuwa wamehifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu na pia watakuwa wamepata utaalamu katika taaluma nyinginezo.

Mufti wa Jimbo la Pahang Sheikh Dr. Abdulrahman Osman amesema Chuo Kikuu cha Al-Qur'an kitatoa fursa mbali mbali za kitaaluma kwa wanachuo ambao watahitimu ambao wote pia watatakiwa kuwa wamehifadhi Qur'ani Tukufu.

Katika Ilani ya 14 ya Uchaguzi Mkuu ya Chama cha Barisan Nasional, moja ya malengo makuu  ni kuweza kuwa na Wamalaysia 125,000 waliohifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu sambamba na kuwa wamehitimu katika taaluma kama vile tiba, hisabati, na uhandisi ifikapo mwaka 2050.

Ilani hiyo inasema Qur'ani Tukufu inatoa muongozo kamili wa sekta zote za maisha na si tu katika masuala yanayohusiana na dini moja kwa moja bali hata katika taaluma kama vile sayansi, teknolojia n.k.

Mufti Osman anasema Qur'ani Tukufu inapaswa kutumika kikamilifu kwa maslahi ya Waislamu duniani.

3465511

captcha