IQNA

Waislamu Milioni 1 wa China katika kambi ya kuwalazimu kufuata Ukomunisti

11:25 - June 12, 2018
Habari ID: 3471554
TEHRAN (IQNA)- Wakuu wa utawala wa China wanawashikilia kwa nguvu Waislamu karibu milioni 1 katika kambi zenye msongamano mkubwa ambapo wanafunzwa kwa lazima itikadi za Kikomunisti.

Taarifa zinasema Waislamu wa jamii ya Uygur wanaoshikiliwa katika kambi iliyo eneo la Xinjiang wanalazimishwa kula nyama ya nguruwe na kunywa pombe.

Katika simulizi za kusikitisha za Mwislamu Omar Bekali ambaye alifanikiwa kuondoka katika kambi hiyo, alilazimishwa kukana itikadi za Kiislamu huku akitakuwa kupongeza Chama cha Kikomunisti cha China lakini alikataa kufanya hivyo na hivyo aliadhibiwa vikali na hatimaye kupelekwa katika gereza kwa muda wa miezi saba. Anabaini kuwa alishikiliwa katika gereza na hakuruhusiwa kupata huduma za wakili pamoja na kuwa yeye ni raia wa Kazakhstan.

Kambi hizo zinalenga kufuta itikadi za Kiislamu na turathi za kiutamaduni miongoni mwa wafungwa na kuwalazimu kufuata itikadi za Kikomunisti. Taarifa inasema kambi hizo zimepanuka kwa kasi katika kipindi cha mwaka moja uliopita na kueneza hofu miongoni mwa Waislamu nchini China. Wanaoshikiliwa katika kambi hizo ni wale wanaoonekana kuwa na kile kinachotajwa kuwa eti ni misimamo mikali ya Kiislamu. Kwa mujibu wa Chama cha Kikomunisti China, watu wenye misimamo mikali ya Kiislamu ni wale ambao huswali misikitini katika siku zisizokuwa Ijumaa, wale ambao huenda kuswali sala za jamaa katika misikiti iliyo nje ya vijiji vyao, au wale ambao wana aya za Qur'ani katika simu zao za mkononi. Hivi karibuni Waislamu 20 wa jamii ya Uyghur walikamatwa na kuadhibiwa vikali waliporejea kutoka katika masomo ya kidini katika moja ya nchi za Mashariki ya Kati.

Kambi hizo-ambazo zinashabihiana na kambi za kulazimisha kufanya kazi za  laogai za zama za Mao-ziko katika eneo la Kahgar katika jimbo la Xinjiang kaskazini magharibi mwa China.

Mkoa wa Xinjiang una wakazi Waisalmu zaidi ya milioni 10 kutoka kabila la Uighur na katika miaka ya hivi karibuni eneo hilo limeshuhudia makabiliano makali baina ya wanajeshi na Waislamu.

Serikali ya China imechukua hatua kadhaa kuwadhibiti Waislamu katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kumteuwa Mkomunisti mwenye misimamo mikali Chen Quanguo kuwa katibu wa chama tawi la Xinjiang tokea mwaka 2016.

3721813

captcha