IQNA

Wanaopanga kuenda Hija wajitayarishe ili wanufaike na safari hiyo ya kipekee

7:25 - July 08, 2018
Habari ID: 3471587
TEHRAN (IQNA)- Afisa wa ngazi za juu wa masuala ya Hija katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito kwa wale waliopanga kutekeleza ibada ya Hija wajitayarishe kikamilifu ili wanufaike kikamilifu na fursa hii nadra katika maisha ya Mwislamu.

Akizungumza hivi karibuni mjini Qum katika hadhara ya wanaopanga kufunga safari ya kutekeleza ibada ya Hija, Hujjatul Islam Sayyid Ali Kadhi Asghar, mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya Hija amesema, Hija ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo wanaopata neema hiyo wanapaswa kunufaika na kila sekunde ya safari hiyo.

"Hija ni safari ya kipekee na baraka na neema zake haziwezi kupatikana katika safari nyinginezo," amesema Sheikh Kadhi Asghar.

Aidha ametoa wito kwa wanaoelekea katika safari ya Hija kuanza kupanga ratiba kamili ya safari hiyo ili waweze kunufaika na malengo matakatifu wanayofuata.

Kwingineko katika hotuba yake, Sheikh Kadhi Asghar amesema matayarisho yanaendelea vizuri ili kuwawezesha Wairani kutekeleza Ibada ya Hija bila matatizo mwaka huu pamoja na kuwa hivi sasa hakuna uhusiano wa kidiplomasia baina ya Saudi Arabia na Iran.

Wairani zaidi ya 85,000 wanatazamiwa kutekeelza Ibada ya Hija mwaka huu ambapo watakuwa Saudia kwa muda wa baina ya siku 28 hadi 45.

Idadi kama hiyo ya Wairani walitekeleza Ibada ya Hija mwaka jana. Mwaka uliotangualia Wairani hawakuweza kutekeleza Ibada ya Hija kutokana na kuzorota uhusiano wa Tehran na Riyadha baada ya maafa ya Mina katika Hija ya mwaka 2015.

Mnamo Septemba 2015, kulijiri msongamano mkubwa wakati wa ibada ya Hija katika eneo la Mina karibu na Makka ambapo duru zisizo rasmi zinasema Mahujaji 7,000 walipoteza maisha huku Saudia ikisisitiza ni watu 770 waliouawa katika msongamano huo. Iran ilitangaza kuwa Mahujaji wake wapatao 465 walipoteza maisha katika maafa hayo ya Mina. Siku kadhaa kabla ya tukio hilo, Mahujaji 100 walipoteza maisha katika Msikiti Mtakatifu wa Makka, wakiwemo Wairani 11 baada ya winchi kuwaangukia wakati wanapotufu.

Maswali mwengi waliibuka kuhusu uwezo wa Saudi Arabia kusimamia zoezi la Hija ambapo mwaka jana Iran ilitaka usalama wa Mahujaji wake udhaminiwe. Kufuatia sisitizo hilo la Iran, Saudi Arabia mwaka 2016 iliwazuia mahujaji Wairani kushiriki katika ibada ya Hija.

3728294

captcha