IQNA

17:44 - September 05, 2018
News ID: 3471660
TEHRAN (IQNA)- Bima ya Kiislamu (Takaful) nchini Kenya imeshuhudia ustawi wa kasi zaidi miongoni mwa mashirika madogo ya bima nchi humo katika mwaka wa 2017.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jumuiya ya Mashirika ya Bima Kenya (AKI), fedha za bima zilizokuswanya na mashirika yenye kufuata mfumo wa Takaful zilifika Ksh milioni 254.52 au takribani dola milioni mbili na nusu ikilinganishwa na Ksh milioni 3.71 tu mwaka 2016.

Mafanikio hayo yamekuja baada Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kusaini sheria mpya ya bima ili kuimarisha nafasi ya Kenya kama kitovu cha mfumo wa fedha wa Kiislamu barani Afrika. Sheria ya Bima (iliyorekebishwa) ya mwaka 2016 iliruhusu mashirika ya bima ya Kiislamu yaani Takaful kufanya kazi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na hivyo kuhimiza mashirika ya kimataifa kuwekeza katika sekta hiyo.  Sheria hiyo mpya ilianza kutekelezwa Januari mwaka jana.

Bima ya Takaful nchini Kenya inatolewa na Shirika la Takaful Insurance of Africa ambalo ndilo shirika pekee lenye kutoa huduma za bima kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu nchini humo. Kati ya mambo mengine, bima ya takaful haitegemei riba na gharar.

Katika miaka ya hivi karibuni huduma za kifedha za Kiislamu zimeimarika nchini Kenya kwa kufunguliwa benki kadhaa za Kiislamu na vile vile benki za kawaida zenye kutoa huduma maalumu kwa mujibu wa sheria za Kiislamu. Inatazamiwa pia mfumo wa bima ya Kiislamu nao pia utastawi kwa kasi nchini Kenya.

Mwaka jana pia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Kenya (CMA) iliruhusu Baraza la Bodi ya Huduma za Kifedha za Kiislamu (IFSB) kuwa mwanachama wa bodi hiyo. IFSB ina makao yake huko Kuala Lumpur Malaysia na ni bodi ya kimataifa inayoweka viwango na kustawisha huduma za kifedha za Kiislamu zenye uwazi na usimamizi bora duniani.

3744200

Name:
Email:
* Comment: