IQNA

Maombolezo ya Muharram yaendelea nchini Kenya

12:32 - September 16, 2018
Habari ID: 3471672
TEHRAN (IQNA)- Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Kenya wanaendelea na maombolezo ya mwezi Muharram katika kukumbuka kuuhawa Shahidi Imam Hussein AS na wafuasia wake katika jangwa la Karbala.

Katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Waislamu Mashia na Waislamu wa madhehebu zingine wanakusanyika katika vituo kadhaa katika Majalis za Muharram. Katika kituo kikubwa zaidi cha Mashia, cha Jaafari Islamic Centre, mawaidha ya Muharram yanatolewa na Sheikh Abdul Jalil Nawee kutoka Ghana kila siku. Aidha katika Msikiti wa Park Road mjini Nairobi, Majlisi za Muharram zimeandaliwa na jumuiya kadhaa kwa pamoja na mawaidha yanatolewa na mashekhe mbali mbali kila siku. Hali kadhalika katika mitaa mingine ya Nairobi kama vile Gachie na Riruta Waislamu Mashia na pia Waislamu wanakusanyika katika majalis za Muharram. Mamombolezo ya mwezi wa Muharram pia yanafanyika katika miji mingine muhimu ya Kenya kama vile, Nakuru, Kisumu, Mombasa, Lamu na Malindi.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 61 Hijria Qamaria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq.

Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi kubwa la batili ili kuilinda dini ya Allah.

Katika siku kumi za kwanza za mwezi wa Muharram, Waislamu, hasa wafuasi wa Madhebu ya Shia na wale wawapendao Ahul Bayt wa Mtume SAW, hushiriki katika hafla mbali mbali za maombolezo ya Imam Hussein AS. Aidha hata wasio kuwa Waislamu katika maeneo mbali mbali pia hujumuika na Waislamu katika maombolezo ya Imam Hussein AS kwani aliuawa shahidi akitetea haki na kupinga udhalimu.

3747008

captcha