IQNA

Tafsiri mpya ya Qur'ani Tukufu yazinduliwa katika ofisi za IQNA

19:59 - December 16, 2018
Habari ID: 3471774
TEHRAN (IQNA)- Tafsiri mpya ya Qur'ani inayojulikana kama 'Tafsiri ya Shams' imezinduliwa katika ofisi za Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) mjini Tehran.

Tafsir ya Shams ya Qur'ani Tukufu imeandikwa kwa lugha ya Kifarsi, ina jildi 10 na imeandikwa na Hujjatul Islam Dkt. Mustafa Boroujerdi na kuchapishwa na Shirika la Uchapishaji la Bustan Kitab.

Hujjatul Islam Boroujerdi ambaye pia hivi sasa ni balozi wa Iran nchini Tunisia ametumia muda wa miaka 11 kuandika na kuhariri tafsiri hiyo ya Qur'ani Tukufu.

Sherehe za uzinduzi wa tafsiri hiyo zimehudhuriwa na wanazuoni na wataalamu wa Qur'ani Tukufu pamoja na maafisa wa kiutamaduni na kisiasa nchini Iran akiwemo Ayatullah Dkt. Seyyed Mostafa Mohaghegh Damad, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyed Abbas Araqchi na Isa Alizadeh mkuu wa masuala ya utamaduni katika Akademia ya Elimu, Utamaduni na Utafiti Iran (ACECR).

Akizungumza katika uzinduzi huo, Araqchi amesema amefanya kazi na Dkt. Boroujerdi  katika wizara ya mambo ya nje kwa muda mrefu na ameitaja Tafsiri ya Shams ya Qur'ani Tukufu kuwa mafanikio makubwa kwani imeandikwa kwa kina na kwa lugha sahali. Amesema uzoefu wa Dkt. Boroujerdi katika wizara ya mambo ya nje ni jambo ambalo limempa ufahamu kuhusu jamii ya kimataifa na hivyo kuboresha zaidi tafsiri hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Dkt. Mohammad Javad Zarif pia ametuma ujumbe katika uzinduzi hiyo ambapo ameashiria nafasi ya Qur'ani Tukufu katika kuwaleta pamoja Waislamu zaidi ya bilioni 1.5 duniani. Aidha amempongeza Dkt. Boroujerdi kwa mafanikio yake ya kuandika Tafisir ya Shams na ametoa wito ifasiriwe kwa lugha muhimu duniani.

Kwa upande wake Ayatullah Mohaghegh Damad amesema kati ya sifa za Tafsiri ya Shams ya Qur'ani Tukufu ni kuwa mwandishi wake amejaribu kufupisha maandishi yake mbali na kuwa amejiepusha na mada zenye kuleta uzushi na mifarakano katika umma wa Kiislamu.Tafsiri mpya ya  Qur'ani yazinduliwa katika ofisi za IQNA

Akizungumza katika uzunduzi huo wa tafsiri aliyoiandika, Hujjatul Islam Dkt. Boroujerdi amesema tarjuma ya Qur'ani Tukufu kwa lugha nyingine huwa kazi ngumu sana na haiwezekani kufikisha maana halisi ya maneno asili ya Kiarabu ya Qur'ani na kwa msingi huo tafsiri huwa na jukumu la kufafanua zaidi aya za Qur'ani.

Dkt. Boroujerdi pia amewahi kuwa balozi wa Iran katika makao makuu ya kanisa katoliki duniani Vatican na pia mwakilishi wa Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC.

3467472

captcha