IQNA

Kiongozi Muadhamu aswalisha Swala ya maiti ya Ayatullah Hashemi Shahroudi

11:43 - December 26, 2018
Habari ID: 3471787
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullahil Udhma Ali Khamenei leo asubuhi ameongoza Swala ya maiti ya marhumu ya Ayatullah Mahmoud Hashemi Shahroudi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran.

Umati mkubwa ukiongozwa na viongozi wa ngazi za juu wa serikali akiwemo Rais Hassan Rouhani, Spika wa bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ali Larijani na Mkuu wa Vyombo vya Mahakama Ayatullah Sadeq Amoli Larijani wameshiriki katika Swala hiyo iliyoswaliwa katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA hapa mjini Tehran.

Mara baada ya kumalizika Swala hiyo ya maiti, ilianza shughuli ya kuusindikiza mwili wa marhumu Ayatullah Shahroudi kuelekea katika mji wa Qum ambapo anatarajiwa kuzikwa katika Haram Tukufu ya Bibi Fatma Maasuma AS.

Ayatullah Shahroudi ambaye wakati wa kifo chake alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo na mkuu wa zamani wa vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliaga dunia Jumatatu jioni akiwa na umri wa miaka 70 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Ayatullah Sayyid Mahmoud Hashemi Shahroudi alizaliwa tarehe 15 Agosti 1948 katika mji wa Najaf nchini Iraq na alikuwa miongoni mwa wanafunzi wakubwa wa shahid Ayatullah Sayyid Muhammad Baqir.

Katika ujumbe wa salamu za rambirambi na mkono wa pole aliotoa leo, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza masikitiko na kubainisha huzuni na majonzi aliyonayo kwa kifo cha Ayatullah Hashemi Shahroudi na kusisitiza kwa kusema: Kuondokewa huku na msiba huu wa kusikitisha uliotokea baada ya karibu mwaka mmoja wa maradhi makubwa na thakili, umewaumiza watu wote wanaoitambua hadhi yake ya kielimu na utumishi wake wenye thamani kubwa kwa Mfumo wa Kiislamu na vile vile kwa taaluma za fiqhi, usuli na sheria katika vyuo vya kidini.

Aidha amemtaja Ayatullah Hashemi Shahroudi kuwa ni alimu mkubwa katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Qum, mtendaji mwaminifu katika chombo muhimu zaidi cha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, mjumbe mwenye taathira kubwa katika Baraza la Walinzi wa Katiba na mwenyekiti aliyefanikiwa katika Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo. Tunamuomba Allah amlaze pema penye wema na amsameh dhambi zake na amjaaliye makao mema ya jannatul firdaus.

3775756

captcha