IQNA

Ujerumani Yatafakari ‘Ushuru wa Msikiti’

12:33 - December 28, 2018
Habari ID: 3471789
TEHRAN (IQNA)- Wabunge katika muungano tawala nchini Ujerumani wamesema wanatafakari kuwashurutisha Waislamu kulipa ‘Ushuru wa Msikiti’ kama ambavyo Wakristo nchini humo wanatozwa ‘Ushuru wa Kanisa’.

Thorsten Frei, mwanachama wa chama cha Christian Democrats (CDU) cha Kansela Angela Merkel amesema siku ya Jumatano kuwa, ‘Ushuru wa Msikiti’ ni hatua muhimu ambayo itaufanya Uislamu nchini Ujerumani usiwe tegemezi kwa misaada ya madola ya kigeni.

Hivi sasa nchini Ujerumani ushuru wa kanisa hukusanya kutoka kwa Wakatoliki na Waprotestanti ili kufadhili shughuli za kanisa. Ushuru wa kanisa hukusanywa na serikali kutoka kwa Wakristo wenye imani na wanaofungamana na mafunzo ya dini yao na kisha fedha hizo hukabidhiwa taasisi za kidini.

Wanasiasa wa chama tawala wanasema kukosekana ushuru kama huo miongoni mwa Waislamu kumepelekea misikiti ya Ujerumani kuwa tegemezi kwa misaada ya kigeni ambayo mingi huja na masharti na hivyo kupenyeza itikadi kali za kidini nchini humo.

Mkuu wa sera za ndani katika chama cha SDP Burkhard Lischka anasema ‘Ushuru wa Msikiti’ utawafanya Waislamu nchini humo wajitegemee na wawe na misimamo huru.

Wakuu wa Ujerumani wana wasiwasi kuhusu ushawishi mkubwa iwa Taasisi ya Kiislamu-Kituruki Ujerumani (DITIB) ambayo inafungamana na idara ya kidini serikali ya Uturuki.

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Horst Seehofer alisema Waislamu ni sehemu ya jamii ya Ujerumani. Aliyasema hayo mwezi Novemba mjini Berlin wakati akizungumza katika Kongamano la Nne la Uislamu nchini Ujerumani (DIK).

Ujerumani ni nchi yenye watu milioni 81 na ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu Ulaya maghairbi baaada ya Ufaransa. Waislamu Ujerumani wanakadiriwa kuwa milioni 4.7 ambapo milioni 3 miongoni mwao wana asili ya Uturuki.

3467545

captcha