IQNA

Wanawake Waislamu Lamu, Kenya wataka marufuku ya Hijabu shuleni iondolewe

14:13 - February 03, 2019
Habari ID: 3471828
TEHRAN (IQNA)- Siku ya Kimataifa ya Hijabu imeadhimishwa Ijumaa katika mji wa Lamu nchini Kenya huku washiriki wakitoa wito wa kuondolewa marufuku ya Hijabu shuleni nchini humo.

Matembezi ya Siku ya Kimataifa ya Hijabu Lamu yaliandaliwa na shirika la kuteteka haki za binadamu la Muslims For Human Rights (Muhuri) ambapo washiriki walijadili uamuzi wa Mahakama ya Kilele Kenya kuidhinisha marufuku ya vazi la Hijabu katika shule nchini humo. Katika hukumu iliyotolewa Januari 24, Mahakama ya Kilele Kenya ilitoa hukumu iliyosema kila shule nchini Kenya ina haki ya kuanisha kanuni za sare na kwa msingi huo shule zimepewa idhini ya kuwanyima wasichana Waislamu haku ya kuvaa Hijabu. Uamuzi huo ulibatilisha uamuzi uliokuwa umetolewa na Mahakama ya Rufaa iliyokuwa imetoa hukumu kuwa wasichana Waislamu wana haki ya kuvaa Hijabu shuleni.
Akizungumza katika Siku ya Kimataifa ya Hijabu, afisa mwandamizi wa Muhuri mjini Lamu Umulkheir Ahmed alisema katiba ya Kenya imebainisha wazi kuwa wananchi wana uhuru wa kuabudu. Amesema sheria inawaruhusu Waislamu kudhihirisha dini kupitia ibada na kutekeleza maamurisho ya dini. Ameongeza kuwa wanawake mjini Lamu wanataka zichukuliwe hatua za kisheria kubatilisha hukumu hiyo ya marufuku ya Hijabu. Bi.Ahmed amesema haki za wasichana Waislamu zitakiukwa iwapo watanyimwa idhini ya kuvaa Hijabu shuleni.
Siku ya Kimataifa ya Hijabu huadhimishwa duniani kote Februari Mosi kwa lengo la kuwahimiza wasio kuwa Waislamu kuvaa Hijabu na ili waweze kufahamu ni kwa nini Waislamu huvaa vazi hilo la staha.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na wimbi kubwa la kupinga Hijabu katika nchi za Magharibi hasa nchini Ufaransa ambapo vazi hilo la Kiislamu limepigwa marufuku katika baadhi ya maeneo ya umma. Aidha pia kumekuwepo na chuki dhidi ya Hijabu katiak nchi zingine duniani zenye kufuata mfumo wa sheria wa Kimagharibi.

captcha